ALAT yaridhishwa ujenzi jengo la utawala Manispaa ya Shinyanga

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 12:51 PM May 09 2025
Mwenyekiti wa ALAT Mkoa wa Shinyanga Mibako Mabubu akizungumzia ujenzi wa Jengo la Utawala Manispaa ya Shinyanga mara baada ya kufanya ziara ya kulikagua pamoja na wajumbe wake.
Picha: Marco Maduhu
Mwenyekiti wa ALAT Mkoa wa Shinyanga Mibako Mabubu akizungumzia ujenzi wa Jengo la Utawala Manispaa ya Shinyanga mara baada ya kufanya ziara ya kulikagua pamoja na wajumbe wake.

Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) Mkoa wa Shinyanga, imeeleza kuridhishwa kwake na maendeleo ya ujenzi wa Jengo la Utawala la Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, wakisema kuwa thamani ya fedha imeonekana kutokana na ubora wa kazi uliofanyika.

Pongezi hizo zimetolewa leo Mei 8,2025, wakati wa ziara ya wajumbe wa ALAT Mkoa,walipotembelea kuona ujenzi wa jengo hilo. 

Mwenyekiti wa ALAT Mkoa wa Shinyanga Mibako Mabubu, amempongeza Mkurugenzi wa Manispaa, Meya na Madiwani, kwa usimamizi bora wa fedha za serikali, akisema jengo linaonyesha mahusiano mazuri baina ya viongozi na wataalamu katika kusimamia miradi ya maendeleo. 

“Jengo tumeliona liko vizuri, lina ubora wa hali ya juu na thamani ya fedha imeonekana,” amesema Mabubu.

 Naye Katibu wa ALAT Mkoa wa Shinyanga Rose Manumba, amempongeza Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha na kujengwa Jengo hilo la Utawala Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, na kuonyesha jinsi gani anavyo jali maslahi ya Watumishi wa Umma, na kuwaweka katika Mazingira mazuri ya utendaji kazi.

“fedha ambazo zimeletwa na Rais Samia zimetumika vizuri katika mradi huu sababu tumejionea sisi wenyewe kwa macho yetu wala hatujasimuliwa,pongezi sana kwa Mkurugenzi wa usimamizi mzuri wa fedha za Rais Samia, Jengo lina ubora,”amesema Rose.

 Mjumbe wa ALAT Mkoa wa Shinyanga Ngassa Mbonje, amesema kwamba fedha za Rais Samia zimetendewa haki katika ujenzi wa Jengo hilo la Utawala, sababu ni zuri na viwango vyake ni bora.

 Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, Alexius Kagunze, amesema jengo hilo litaongeza ufanisi wa utendaji kazi, kwa kuwaunganisha watumishi katika eneo moja na kuwezesha wananchi kupata huduma kwa wakati. 

Awali Kaimu Mkuu wa Divisheni ya Mipango na Uratibu  Manispaa ya Shinyanga Paschal Hyera, akisoma taarifa ya ujenzi huo, amesema ulianza Aprili 14, 2022 kwa njia ya Force Account kwa kutumia mafundi wa ndani, na unatarajiwa kukamilika Desemba 30,2025 kwa gharama ya sh.bilioni 4 fedha kutoka serikali kuu. 

Amesema Jengo hilo lina ghorofa mbili, ofisi 41, kumbi mbili za mikutano, vyumba vitano vya TEHAMA, matundu 14 ya vyoo,na kwamba mradi huo umefikia asilimia 89 ya utekelezaji,ambapo kazi zilizobaki ni ukamilishaji wa skimming ndani na nje, ufungaji wa mifumo ya TEHAMA, umeme, maji, ujenzi wa partition na uwekaji wa vigae.