Bazara la Ardhi na Nyumba Moshi, limeumaliza mgogoro wa ardhi wa muda mrefu, kati ya mfanyabiashara maarufu nchini, Frank Marealle na ndugu yake Acley Marealle, baada ya kutoa hukumu iliyompa ushindi Acley Marealle.
Mfanyabiashara huyo Frank Marialle (mleta maombi), alifungua maombi Namba 51 ya Mwaka 2020 katika baraza hilo, akiomba atamkwe ndiye mmiliki wa ardhi iliyoko Kijiji cha Lyamrakana, Marangu, Wilaya ya Moshi.
Aidha mleta maombi (Frank Marialle), alikuwa akiomba mwili wa Veronica David Mlang’a, ambaye alikuwa mke wa Mangi David Mlang’a Marialle, uliozikwa katika ardhi yenye mgogoro ufukuliwe; pia alikuwa akiomba mjibu maombi kubeba gharama za kesi.
Akizungumza nje ya baraza hilo, baada ya kutolewa hukumu hiyo, Julius Semali, ambaye ni Wakili wa mjibu maombi (Acley), alidai kuwa mahakama imetoa hukumu kwamba, Frank David Marialle, sio mmiliki halali wa ardhi yenye mgogoro; na kwamba mmiliki halali ni Acley Marealle.
Hukumu hiyo imesomwa leo (Mei 9, 2025) na Mwenyekiti wa Baraza hilo la Ardhi na Nyumba Moshi, Hussein Lukeha.
Aidha, Wakili Semali, ameeleza kuwa mahakama hiyo, imetoa amri kuwa mwili wa Veronica Mlang’a Marialle usifukuliwe; na kila upande ubebe gharama zake.
Frank Marialle, alikuwa akidai anamiliki kihalali ardhi hiyo tangu mwaka 1931, kupitia kwa mama yake, aitwaye Asinath Marealle, aliyekuwa miongoni mwa wake wa Mangi David Marealle.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED