Rais Samia kuongoza mazishi ya hayati Msuya Mei 13

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 08:24 PM May 09 2025
Rais Samia kuongoza mazishi ya hayati Msuya Mei 13
Picha: Mpigapicha Wetu
Rais Samia kuongoza mazishi ya hayati Msuya Mei 13

Rais Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuongoza waombolezaji katika mazishi ya aliyewahi kuwa Makamu wa Rais wa Kwanza na Waziri Mkuu mstaafu, Hayati Cleopa Msuya, kijijini kwao Usangi Mwanga mkoani Kilimanjaro Mei 13, mwaka huu.

Akitoa ratiba ya mazishi hayo leo Dar es Salaam, Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa, amesema kesho Jumamosi mwili wa marehemu utapelekwa nyumbani kwake kwa taratibu za kifamilia.

Amesema siku ya Jumapili Mei 11 Rais wa Samia anatarajiwa kuwaongoza Watanzania katika Ibada ya kuombea mwili wa marehemu itakayofanyika katika viwanja vya Karimjee, Ilala Dar es Salaam kuanzia saa 3:00 asubuhi.

"Ibada hiyo itakayoambatana na salamu pamoja na kuaga mwili wa Hayati Msuya katika viwanja hivyo vitafanyika kuanzia majira ya saa 03 asubuhi hadi saa 07 mchana.

"Siku ya Jumatatu Mei 12 mwili wa Hayati Msuya utasafirishwa kwa ndege kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanga Kilimanjaro kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), tunatarajia mwili utawasili na kupokelewa KIA kati ya saa 2:30 na saa 3:30 asubuhi," amesema Msigwa.

Ameongeza kuwa baada ya kuondoka KIA, mwili wa marehemu utasafirishwa kwa magari na kupelekwa katika uwanja wa Cleopa Msuya uliopo Mwanga ambako viongozi mbalimbali na wananchi watapata fursa ya kuuaga.

"Tunatarajia ratiba ya kuaga katika uwanja huu, itaanza majira ya saa 5:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni siku ya Jumatatu, Mei 12," amebainisha Msigwa.

Pia Msigwa ametoa wito kwa wananchi wa Mwanga na maeneo mengine wanaotaka kumuaga mpendwa wao Hayati Msuya kutumia nafasi hiyo iliyotengwa kwa ajili yao kumuaga, na kwamba baada ya saa 10 jioni mwili utapelekwa kijijini kwao Usangi ambako kutakuwa na Ibada fupi ya maombolezo.

Amesema siku ya Jumanne Mei 13, ndiyo itakuwa siku ya mazishi ambako ratiba itaanza kwa Ibada maalum itakayofanyika katika Kanisa la KKKT lililopo Usangi itakayofuatiwa na mazishi ya kiserikali nyumbani kwake yatakayoongozwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

"Baada ya mazishi kutakuwa na salamu za viongozi wachache akiwemo Rais Samia," amesema.