Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kwa kushirikiana na wataalamu wa teknolojia kutoka nje ya mipaka ya Tanzania wanatarajia kuanza kutoa mafunzo kwa walimu na wakuza mitaala kwa kutumia Akili Mnemba (AI) wakilenga kuongeza ufanisi katika ufundishaji na ujifunzaji.
Akizungumza leo mkoani Dar es Salaam wakati wa hafla ya utiaji saini makubaliano hayo katika ya TET na taasisi ya Tanzania AI Community, Mkurugenzi Mkuu wa TET Dk. Aneth Komba amesema jukumu la taasisi hiyo litakuwa ni kutoa mafunzo ya kukuza uwezo wa wakuza mitaala na walimu wote nchini kwa kutumia AI.
Amesema kwa upande wa TET jukumu lao kubwa litakuwa ni kuhakikisha kwamba wadau hao wa teknolojia wanapata karikulam, silabasi na vitabu ili viweze kuwasaidia kutumia AI katika ufundishaji na ujifunzaji.
"Kwetu tunaona ni mapinduzi makubwa kwa sasa duniani kuna maendeleo makubwa sana katika sayansi na teknolojia kwahiyo matumizi ya Akili Mnemba AI katika ufundishaji na ujifunzaji yatampunguzia sana mzigo mwalimu.
"Nimeona ni ukombozi na utamsaidia sana mwalimu kumpunguzia mzigo lakini pia kuimarifa ufundishaji na ujifunzaji kwa watoto wetu ambao ndio vijana wanaokuja kuuishi ulimwengu wa sayansi na teknolojia," amesema Dk. Aneth.
Ameongeza kwa kuishukuru Tanzania AI Community kwa kuwa tayari kushirikiana nao akieleza kuwa Taasisi ya Elimu wako tayari kutimiza majukumu yao. "Mkataba utakuwa wa miaka mitatu na baada ya kutamatisha muda huo tutakiwa na kipindi cha kufanya upembuzi yakinifu kuona tulifanikiwa wapi, na tumekwama wapi na tunaweza kurudia tena".
Aidha, ameeleza kiwa lengo lao ni kuhakikisha kwamba wanawafiki walimu wote nchini wanaoweza kutumia teknolojia hiyo katika jirahisisha ufundishaji na ujifunzaji, na kwamba katika mtaa mpya wataingiza kipengele cha kutumia AI katika ifundishaji na ujifinzaji.
Naye, Mkurugenzi wa Tanzania AI Community, Essa Mohamedal, alisema wamefurahi kushirikiana na Taasisi ya Elimu kwakuwa wataweza kuwaongezea uwezo walimu wote nchini na kuwafanya watekeleze vizuri zaidi majukumu yao.
"Tuko hapa kwaajili ya kuwapatia walimu zana muhimu zitakazowasaidia kufundisha wanafunzi kwa ufanisi zaidi, na tunafurahisana kushirikiana na TET katika kuhakikisha AI inatumika kuleta mapinduzi ya elimu nchini," amesema Mohamedal.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED