Katibu G55, wenzake watimka CHADEMA, walalama chama kimepoteza mwelekeo

By Imani Nathaniel , Nipashe
Published at 03:16 PM May 09 2025
Katibu G55, wenzake watimka CHADEMA, walalama chama kimepoteza mwelekeo
Picha: Imani Nathaniel
Katibu G55, wenzake watimka CHADEMA, walalama chama kimepoteza mwelekeo

Aliyekuwa Katibu wa Watia Nia wa Ubunge kupitia kundi maarufu la G55, Edward Kinabo, ametangaza rasmi kujivua uanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), akidai kuwa chama hicho kimepoteza dira ya kidemokrasia na misingi yake ya awali.

Kinabo ametoa tamko hilo Mei 9, 2025, katika mkutano na waandishi wa habari, akieleza kuwa hali ya ndani ya CHADEMA imekuwa tete kuliko changamoto zinazowakabili kutoka nje ya chama.

“Ndani ya chama chetu hali si shwari. Wahenga walisema, mficha maradhi kifo humuumbua. CHADEMA si chama kile tena tulichokijenga. Kimepoteza mwelekeo na sasa kinatoka kabisa kwenye mstari wa vyama vya siasa vyenye msingi wa kidemokrasia,” amesema Kinabo.

Akiendelea kufafanua, amesema kujitoa kwake hakumaanishi kuwa haamini tena katika falsafa na itikadi za kweli za kisiasa, bali ni hatua ya kuendeleza harakati hizo kupitia vyama vingine.

“CHADEMA sasa kina makundi mawili ndani ya chama kimoja. Uongozi umeshindwa kukiunganisha chama na wanachama. Huu siyo mwelekeo tuliotarajia,” ameongeza.

Kinabo amesema amekuwa mwanachama wa CHADEMA kwa zaidi ya miaka 20, tangu akiwa chuoni, na ametumikia chama hicho kwa nyadhifa mbalimbali kwa muda mrefu. Hata hivyo, alieleza kuwa juhudi za kuishauri chama zimekuwa zikipuuzwa, huku wapinzani wa maoni tofauti wakionekana kama wasaliti.

“Mpango wa chama kujaribu kuzuia uchaguzi ni hatari kwa taifa. Badala ya kushiriki na kushinda kwa hoja, wanatoa wito wa kususia uchaguzi. Hii siyo demokrasia, na tukisema ukweli tunaonekana wasaliti,” ameeleza.

Aidha, Kinabo ameelezea masikitiko yake kuhusu namna mwenyekiti wa chama, Freeman Mbowe, anavyodhalilishwa ndani ya chama na baadhi ya wanachama, huku akidai kuwa wale wanaomuunga mkono Mbowe wanaonekana kama waasi.

Kwa upande wake, aliyekuwa Mjumbe wa Mkutano Mkuu Wilaya ya Temeke, Eliya Evalist, naye ametangaza kujivua uanachama na nyadhifa zote ndani ya CHADEMA, akilalamikia kile alichokiita “chuki na mgawanyiko usiomalizika” ndani ya chama.

“Wanasema tumenunuliwa, lakini Heche si tofauti na 'madalali' wengine. Gari analotumia kadi yake inasomeka kwa jina la mke wa Waziri mmoja kutoka CCM. Hii ni aibu kwa chama kinachojinasibu kuwa cha mabadiliko,” amesema Evalist.

Naye Salma Sharifu, aliyekuwa Mjumbe wa Mkutano Mkuu kupitia Baraza la Wanawake CHADEMA (BAWACHA) Taifa, ameeleza kuwa ameondoka ndani ya chama hicho kwa maumivu makubwa, baada ya kulitumikia kwa damu na jasho.

“Nilinyanyaswa na kubaguliwa kwa kuwa upande wa Mbowe. Nimepoteza ndugu zangu kwa sababu ya CHADEMA. Huu siyo upinzani wa kweli tena. Naamini muda umefika wa kuendelea na harakati mahali pengine,” amesema Salma kwa hisia.

Viongozi hao wametoa wito kwa wanachama wengine waliopitia mazingira kama yao kuungana nao katika kuendeleza harakati za kisiasa kwa njia nyingine nje ya CHADEMA.