Mradi Kituo cha Kupoza Umeme Mabibo wakamilika 90%

By Pilly Kigome , Nipashe
Published at 03:58 PM May 09 2025
Kamati ya Siasa Mkoa wa Dar es Salaam walipotembelea mradi huo uliopo katika Halmashauri ya Ubungo.
Picha: Pilly Kigome
Kamati ya Siasa Mkoa wa Dar es Salaam walipotembelea mradi huo uliopo katika Halmashauri ya Ubungo.

Kituo cha mradi wa uimarishaji wa kupoza umeme wa gridi ya Taifa cha Mabibo Wilayani Ubungo unaokwenda kuondoa changamoto za kukosekana kwa umeme umekamilika kwa asilimia 90 unatarajiwa kukamilika mwezi Novemba 2025.

Hayo yamesemwa Mei 8, 2025 na Meneja Mradi TANESCO , Mha. Josephat Mwaseke alipokuwa akitoa taarifa fupi kwa Kamati ya Siasa Mkoa wa Dar es Salaam walipotembelea mradi huo uliopo katika Halmashauri ya Ubungo.

Eng.Mwaseke amebainisha mradi huo unafadhiliwa na Serikali ya Tanzania utagharimu  Shilingi Bilion 125 na utakuwa na jumla transifoma nne ambazo kutakuwa na njia kuu mbili kubwa ambayo ile ya MVA 200 na MVA 90 ambazo zitawezesha kulishia wateja wa mkoani Dar es Salaam.

Meneja wa TANESCO Kinondoni Kusini Florence Mwakasege alisema mradi huo unakwenda kuwakomboa wana Dar es Salaam kuepukana na adha ya kukosa umeme na utakwenda kuleta tija na faida kubwa kwa wakazi wa jiji.

Alisema line hizo mbili zitakazokuwa katika kituo hicho zitakwenda kusambaza umeme wa wakazi wa jiji na kutakuwa na umeme wa uhakika.

“Umeme huu utakaofika hapa utatokea kituo cha Kinyerezi na utafika hapa kupozwa na kusambazwa kwa wateja” alisema

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dar es Salaam, Abbas Mtemvu alikitaka kituo hicho kikamilke kwa wakati na kiende kukomboa wananchi kwani tatizo la umeme limekuwa ni changamoto kubwa inayowakabili wakazi wa jiji.

Katika ziara hiyo Kamati hiyo ya Siasa ya Mkoa wa Dar es Salaam waliweza kutembelea mradi wa Booster DAWASA Kibamba, kukagua mradi wa vyumba vinne(4) vya madarasa na matundu nane(8) ya vyoo Shule ya Sekondari Mbezi Inn na pia kukagua Mradi wa ujenzi  wa jengo la upasuaji na wodi ya wazazi kituo cha afya Makurumla.

Akiwa katika Shule ya Sekondari Mbezi Inn Abbas Mtemvu alitoa maagizo kuongeza juhudi katika kuboresha elimu katika shule hiyo waweze kuondoa ziro na divisheni four kwakuwa shule hiyo kumekuwa na matokeo mabaya ambayo hayaridhishi.

“Ni lazima muwe na uchungu na fedha zinazotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan anavyowekeza kwenye elimu kwani anatoa fedha nyingi kuboresha elimu lakini kumekuwa hakuna mafanikio ni lazima muwekeze mpambane muondoe ziro ambazo zimefikia 30 kwa matokeo yaliyopita” alisema

Aidha alipotembelea ujenzi wa jengo la upasuaji na uzazi katika Kata ya Makurumla hakupendezwa na maendeleo ya ujenzi huo kwa kugundua kuna uzorotaji wa kukamilika kwa ujenzi huo na kukosa usimamizi wa kina katika ujenzi huo.

Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Albert Msando alitoa maagizo kwa watendaji wote waweze kufanya kazi kwa weledi na juhudi kubwa kwakuwa hatokuwa na mchezo na mtu yoyote ambae ataleta mizaha kwenye kazi.

“Mimi sihitaji chawa kama kuna mtu anajindaa labda awe chawa wangu sihitaji na wala sihitaji makundi na sitegemei kuwa na kundi, mimi nataka tufanye kazi ya kweli tuiendeleze Ubungo na kama kuna mtu anasema mimi mgeni mimi sio mgeni mimi ni Mkuu wa Wilaya ya Ubungo” alisema