Mratibu Kitaifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Wakili Onesmo Olengurumwa, amelishauri Jeshi la Polisi kutoa taarifa rasmi kwa umma kuhusu mahali walipo wanahabari Boniface Mwangi kutoka Kenya na Agatha Atuhaire wa Uganda, ili kuondoa usiri unaozua taharuki na chokochoko zisizo na ulazima, ambazo zinaweza kuathiri taswira ya taifa kimataifa.
Akizungumza leo Mei 21, 2025 jijini Dar es Salaam, Olengurumwa alisema ukimya uliopo kuhusu wanahabari hao walioripotiwa kukamatwa na kushikiliwa katika Kituo Kikuu cha Polisi jijini Dar es Salaam tangu Mei 18, unavunja taratibu za kisheria za haki za binadamu, kwa kuwa sheria inaelekeza kuwa kila mtu aliye kizuizini apewe haki ya kupata msaada wa kisheria na kufikishwa mahakamani kwa wakati.
“Sheria zetu na viwango vya kimataifa vinataka haki za watu walioko kizuizini ziheshimiwe. Hata kama wanahabari hawa wana tuhuma za kujibu, taratibu za kisheria zichukue mkondo wake. Wasipofikishwa mahakamani, warudishwe kwao kwa heshima,” amesema Olengurumwa.
Ameeleza kuwa Mei 20, 2025 zilisambaa taarifa kwamba wanahabari hao wamerudishwa kwenye nchi zao, lakini baada ya ufuatiliaji wa karibu ilibainika kuwa hawakurudishwa, hali inayoongeza sintofahamu na kuzua mashaka kuhusu mwenendo wa taasisi za dola.
Wakili Olengurumwa pia amebainisha kuwa kuzuiwa kwa mawakili kuonana na wanahabari hao ni ukiukwaji wa wazi wa haki za msingi, jambo linalotia doa taifa kimataifa na kuzua taswira kuwa Tanzania haitii maanani misingi ya utawala wa sheria na haki za binadamu.
“Kitendo hiki kinajenga picha mbaya nje ya nchi. Tunasisitiza matumizi ya busara kumaliza suala hili bila kulidhalilisha taifa,” ameongeza.
Olengurumwa ameongeza kuwa endapo Jeshi la Polisi halitachukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria, THRDC itawasilisha maombi rasmi Mahakamani ili mamlaka husika zitoe tamko au kuelekeza hatua zinazostahili kuchukuliwa.
“Usiri huu unaweza kusababisha madhara makubwa ikiwa ni pamoja na madai ya mateso. Hali kama hii si vyema ikatokea kwa wageni walioko nchini kwetu,” amesema.
Katika taarifa yake ya Mei 19, 2025, THRDC ilitoa wito kwa Jeshi la Polisi kuheshimu viwango vya kimataifa vinavyolinda haki za binadamu, hasa kwa watu walioko kizuizini.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED