Wakili Majaliwa awania urais kupitia Chama cha NRA

By Grace Gurisha , Nipashe
Published at 01:22 PM May 21 2025
Wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mohamed Majaliwa.
Picha: Mpigapicha Wetu
Wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mohamed Majaliwa.

Wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mohamed Majaliwa, ametangaza nia ya kuwania urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha National Reconstruction Alliance (NRA), kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

Majaliwa amekabidhiwa rasmi fomu ya kuomba kuteuliwa kuwa mgombea wa urais leo, Mei 21, 2025, jijini Dar es Salaam na Katibu wa Kamati ya Uchaguzi wa chama hicho, Twaha Kambaya.

Akizungumza mara baada ya kupokea fomu hiyo, Majaliwa ambaye pia ni Kaimu Mwenyekiti wa NRA, amesema amefikia uamuzi huo baada ya kujitathmini kwa kina na kubaini kuwa anayo uwezo, sifa na dhamira ya kweli ya kuwatumikia Watanzania katika nafasi ya juu ya uongozi wa nchi.

“Nimejiangalia na kujiridhisha kuwa mimi ni miongoni mwa Watanzania wanaostahili kukalia kiti cha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Naahidi kuwa endapo nitapewa ridhaa na wananchi, nitatekeleza kwa dhati vipaumbele vyangu vitano ambavyo ni nguzo ya maendeleo ya Taifa letu,” amesema Majaliwa.
Wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mohamed Majaliwa

Vipaumbele Vyake Vitano

1. 📚 Elimu:
Majaliwa amesema hataridhika hadi mfumo wa elimu nchini ubadilike na kutoa huduma bora kwa kila Mtanzania. Ameeleza dhamira yake ya kusimamia kikamilifu sekta hiyo ili kuhakikisha elimu inakuwa chombo cha kweli cha ukombozi na maendeleo.

2.🌽 Kilimo:
Kipaumbele cha pili ni kilimo. Majaliwa amesema atahakikisha kuwa sekta ya kilimo inachangia ipasavyo katika uchumi wa taifa, akisisitiza kuwa Tanzania imejaliwa ardhi na hali ya hewa nzuri ambazo hazijatumika kikamilifu.

3. 👨🏻‍🤝‍👨🏽 Vijana:
Kipaumbele cha tatu ni kwa vijana wa Tanzania. Majaliwa amesema vijana ndio nguzo kuu ya maendeleo, hivyo atahakikisha wanapewa nafasi ya kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi, kijamii na kisiasa ili kulisukuma gurudumu la maendeleo ya taifa.

4. 🚆 Rasilimali za Taifa:
Amesema hataridhika na jinsi rasilimali za nchi – ikiwemo madini na maliasili – zinavyotumika kwa sasa. Ameahidi kusimamia kwa makini sekta hiyo ili kuhakikisha kila Mtanzania anafaidika na utajiri wa taifa lake.

5. 📝 Usalama wa Raia:
Kipaumbele cha tano ni usalama wa raia. Majaliwa amesema ili taifa litawalike na wananchi wake waweze kuzalisha mali kwa ustawi wao binafsi na wa nchi kwa ujumla, ni lazima kuwepo kwa amani na ulinzi wa kutosha kwa kila mmoja.

“Chini ya ilani ya NRA tutakayotangaza, tutahakikisha tunatumia mbinu mbadala na madhubuti ili kila Mtanzania awe salama na ajivunie taifa lake, chini ya uongozi wangu iwapo nitachaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” amesisitiza Majaliwa.
Wakili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mohamed Majaliwa kulia.