Wamiliki na madereva wa pikipiki za miguu mitatu zinazotumia nishati ya umeme, maarufu kama maguta, wametakiwa kusajili na kurasimisha vyombo vyao ndani ya siku 30 ili waendelee na shughuli zao kwa kufuata sheria na taratibu.
Agizo hilo limetolewa leo Mei 21, 2025 na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, wakati wa mkutano uliofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam, uliowakutanisha madereva na wamiliki wa maguta hayo.
“Ni lazima kila mmoja awe na leseni maalum kutoka LATRA, bima halali na kuzingatia sheria za usalama barabarani. Lengo letu ni kuhakikisha mnaendesha shughuli zenu kwa utaratibu na kwa uhuru pasipo bugudha,” amesema DC Mpogolo.
Mpogolo alieleza kuwa katika eneo la Kariakoo pekee kuna zaidi ya maguta 3,500 yanayoendesha shughuli za kusafirisha mizigo bila kuwa na utaratibu wowote rasmi, jambo linalosababisha msongamano, uharibifu wa miundombinu na kero kwa wafanyabiashara na wananchi.
“Rais Samia Suluhu Hassan ametoa maelekezo ya kulisaidia kundi hili. Nendeni darasani, mkomeshe utaratibu wa kiholela. Huu ni wakati wa kuchangamkia fursa,” amesisitiza.
Naye Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, El-Huruma Mabelya, amesema mpango wa kuwasajili waendesha maguta na kuwarasimisha unalenga kuwaweka katika mfumo rasmi ili kuondoa kero zinazoletwa na vyombo hivyo hasa katika maeneo nyeti kama Kariakoo.
“Tutawapangia maeneo rasmi ya kuegesha maguta na atakayekaidi taratibu sheria itachukua mkondo wake. Kariakoo ni soko la kimataifa linahitaji mpangilio, usafi, usalama na hadhi,” amesema Mabelya.
Afisa Mfawidhi wa LATRA Mkoa wa Dar es Salaam, Ngeleza Pateli, amesisitiza kuwa kila mmiliki na dereva wa guta anatakiwa kupatiwa namba ya usajili na dereva awe na leseni halali ya kuendesha chombo hicho.
“Kupitia utaratibu huu, kila mmoja atapata elimu ya njia salama za kutumia barabara, na kwa pamoja tutaimarisha usafiri wa mizigo jijini,” amesema Pateli.
Baadhi ya madereva wa maguta waliohudhuria mkutano huo walieleza kuwa wako tayari kufuata maagizo hayo ya serikali, lakini waliomba waongezewe muda zaidi ili kukamilisha taratibu za usajili na kupata leseni.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED