Mtoto wa siku tisa aliyeibwa Mbeya apatikana akiwa hai

By Grace Mwakalinga , Nipashe
Published at 05:10 PM May 21 2025
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga.
Picha: Mtandao
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya, kwa kushirikiana na wananchi wa Mtaa wa Iyela One, limefanikiwa kumpata mtoto mchanga wa siku tisa, aitwaye Isaka Ambwene, ambaye aliripotiwa kuibwa na watu wasiojulikana.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga, tukio hilo lilitokea Aprili 29, 2025, kufuatia taarifa iliyotolewa na Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Iyela One, Ambakisye Kilundu (46), kuhusu kutoweka kwa mtoto huyo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kamanda Kuzaga amesema mama mzazi wa mtoto huyo, Neema Mkunywa (22), mkazi wa Iyela One, alieleza kuwa siku ya tukio alitembelewa na dada yake, Rukia Mohamed (27), mkazi wa Iyela. Baada ya kumkaribisha, aliamua kumsindikiza, na kwa muda huo alimwacha mtoto wake peke yake ndani ya nyumba akiwa amelala, huku mlango ukiwa umefungwa.

Aliporejea nyumbani, alimkuta mume wake, Ambwene Adam (25), tayari amerudi, lakini mtoto hakuwepo. Hali hiyo ilisababisha taharuki na taarifa kutolewa kwa vyombo vya dola.

Mtoto Apatikana Akiwa Hai

Kamanda Kuzaga ameeleza kuwa baada ya juhudi za kina za upelelezi, mnamo Mei 15, 2025, majira ya saa tatu usiku, mtoto alikutwa akiwa hai na ametupwa nje karibu na nyumba ya wazazi wake.

"Mtoto alikutwa akiwa hai nje ya nyumba jirani na anayoishi baba na mama yake mzazi. Jeshi la Polisi linaendelea na upelelezi ili kuwatambua na kuwasaka waliohusika na tukio hili kwa ajili ya kuchukua hatua za kisheria," amesisitiza Kamanda Kuzaga.

Wito kwa Wananchi

Jeshi la Polisi limetoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwa wahusika wa tukio hilo, huku likiahidi kuendelea kuchukua hatua kali kwa yeyote atakayebainika kujihusisha na matukio ya namna hiyo.