Shirika la Amref Health Africa Tanzania (Amref Tanzania) kwa kushirikiana na Serikali kupitia wizara ya Afya limezindua rasmi mradi wa kuboresha huduma kwa watu wanaoishi na kifafa pamoja na matatizo mengine ya mfumo wa fahamu.
Mradi huo uitwao “Enhancing Epilepsy Care in Africa (EECA)” umezinduliwa Mkoa wa Dodoma, ukilenga Wilaya za Bahi na Chamwino kama maeneo ya mfano kwa utoaji wa huduma jumuishi za kifafa zinazoendeshwa kwa kushirikisha jamii.
Mradi huu wa miaka mitatu, unaotekelezwa kuanzia Januari 1, 2025 hadi Desemba 30, 2027, Kwa ushirikiano kati ya Amref Tanzania, Wizara ya Afya, OR-TAMISEMI, Asasi isiyokuwa ya Kiserikali inayojihusisha na kuijengea jamaa uelewa juu ya Kifafa Tanzania (TEA), Asasi isiyokuwa ya Kiserikali ya Wazazi wa Watoto Wenye Kifafa Tanzania (POCET), Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) na Chuo Kikuu Antwerp cha Ubeligiji. Ufadhili wa mradi huu umetolewa na BAND Foundation na kuungwa mkono na UCB Innovation for Health Equity Fund.
Mradi unalenga makundi mbalimbali katika jamii ikiwemo wananchi kwa ujumla, watu wenye kifafa, wazazi, walezi, familia, watoa huduma za afya, watunga sera, pamoja na viongozi wa kijamii.
Mpango huo ni mojawapo ya jitihada za Shirika la Amref Tanzania katika kushirkiana na Serikali na wadau mbalimbali katika kuboresha Mifumo Imara ya Afya (HSS) na Kuwawezesha Wananchi kwa lengo la kufanikisha huduma endelevu za afya zinazomlenga mwananchi.
Vilevile kuboresha huduma bora za kifafa na matibabu, kupitia mafunzo kwa wahudumu wa afya, kampeni za kupambana na unyanyapaa. Vilevile mradi unalenga kuboresha afya, ubora wa maisha na ujumuishwaji wa watu wenye kifafa pamoja na familia zao katika jamii husika.
“Mradi wa EECA ni hatua muhimu katika utekelezaji wa dhamira ya Shirika la Amref Tanzania ya kushiriki katika kuimarisha mifumo ya afya na kuwawezesha wananchi,” alisema Dkt. Aisa Muya, Mkurugenzi wa Programu - Amref Tanzania na kuongeza kuwa;
“Kwa kuboresha huduma za kifafa katika mfumo wa afya ya msingi nchini, tutaboresha upatikanaji wa huduma za matibabu huku tukijenga uhimilivu na umiliki wa huduma hizi katika jamii. Hii ni sehemu ya mkakati wa Shirika katika kuboresha mifumo ya huduma za Afya kama kifafa. Mradi huu unaakisi mkakati wetu mpana wa Kuimarisha Mifumo ya Afya kwa kuwekeza katika rasilimali watu, matumizi ya takwimu, utoaji wa huduma, na uongozi wa kijamii ili kujenga mfumo wa afya jumuishi na wenye usawa zaidi.”
Akizindua rasmi mradi huo, Kaimu Mkurugenzi Tiba, Wizara ya Afya, Dk. Winifrida Kidima, ameeleza umuhimu mkubwa wa mradi huo kwa taifa.
“Mradi huu ni hatua ya mabadiliko katika namna tunavyokabiliana na matatizo mengine ya mfumo wa fahamu kama kifafa,” alisema Dkt. Kidima “Ni wajibu wetu kama jamii kushirikiana kuondoa unyanyapaa, kuvunja ukimya, na kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma na msaada wa kijamii wanaohitaji.”
Mradi wa EECA utatekelezwa kwa kuzingatia mfumo wa huduma za afya ya msingi nchini (PHC), ili kuhakikisha uendelevu wa muda mrefu, umiliki wa ndani na ulinganifu wa sera. Kipengele kikuu kitakuwa kuendesha kampeni dhidi ya unyanyapaa, kuhamasishaji jamii, pamoja na mafunzo kwa wahudumu wa afya, wahudumu wa afya ngazi ya jamii (CHWs), walezi na viongozi wa kijamii.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED