Jubilee yazindua Akiba Flex, serikali yataka madai kulipwa kwa wakati

By Mary Kadoke , Nipashe
Published at 02:47 PM May 21 2025
Naibu Kamishna wa Bima Khadija Said, (wa pili kushoto) akisikia maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Bima ya Maisha ya Jubilee Helena Mzena, (wa pili kulia) wakati wakielekea kuzindua mpango wa bima ya maisha jijini Dar es Salaam jana.
PICHA: MARY KADOKE
Naibu Kamishna wa Bima Khadija Said, (wa pili kushoto) akisikia maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Bima ya Maisha ya Jubilee Helena Mzena, (wa pili kulia) wakati wakielekea kuzindua mpango wa bima ya maisha jijini Dar es Salaam jana.

SERIKALI imetoa wito kwa kampuni za bima ya maisha kuhakikisha wanalipa madai kwa wakati, ikionya kuwa ucheleweshaji unazinyima familia zinazokabiliwa na misiba faraja ya kifedha wakati wa majonzi.

Kauli hiyo ilitolewa jijini Dar es Salaam na Naibu Kamishna wa Bima, Khadija Said, wakati wa uzinduzi rasmi wa Mpango wa Akiba Flex ulioanzishwa na Bima ya Maisha ya Jubilee – mpango wa bima ya maisha unaolenga watu wenye mahitaji ya kifedha ya muda mrefu.

Akisisitiza umuhimu wa ulipaji wa madai kwa haraka, Khadija alisema kampuni za bima ya maisha hazina budi kuhakikisha zinashughulikia madai kwa wakati, kwani kuchelewa kunaleta mzigo zaidi kwa familia zinazopitia matatizo ya kifedha na kihisia.

“Makampuni ya bima ya maisha lazima yashughulikie madai kwa haraka, kwani ulipaji wa wakati ni muhimu ili kutoa msaada wa kifedha wa haraka kwa familia zinazokumbwa na majonzi. Kushindwa kufanya hivyo kunazidisha mateso yao na pia kunapunguza imani ya wananchi katika sekta ya bima,” alisema.

Aliongeza: “Naamini Mpango wa Akiba Flex utakuwa mkombozi kwa familia nyingi, ukiwapatia usalama wa kifedha na utulivu wa akili wakati wa changamoto.”

Mkurugenzi Mtendaji wa Bima ya Maisha ya Jubilee Helena Mzena, alisema AkibaFlex ni sehemu ya juhudi za kampuni hiyo kujaza mapengo ya soko kwa kutoa suluhisho linalowezesha wateja kukidhi mahitaji yao ya uwekezaji na ulinzi wa kifedha.

“AkibaFlex ni taswira ya uelewa wetu wa kina kuhusu mteja wa kisasa wa Kitanzania — mtu anayethamini ulinzi wa bima ya maisha lakini pia anahitaji kuwa na uwezo wa kupata fedha zake panapotokea fursa au dharura,” alisema.

“Ni kuwapa wateja wetu udhibiti, kuwawezesha kupanga kwa busara na kuishi kwa kujiamini. Tunajivunia kuongoza katika kutoa suluhisho bunifu na jumuishi linalogusa mahitaji halisi ya maisha,” aliongeza.

Licha ya ukuaji wa hivi karibuni katika sekta hiyo, uelewa na matumizi ya bima ya maisha bado ni mdogo nchini Tanzania. Kwa mujibu wa Taasisi ya Maendeleo ya Sekta ya Fedha Tanzania (FSDT), ni asilimia 10 pekee ya Watanzania walio na aina yoyote ya bima rasmi.

Sekta ya bima imeendelea kukua nchini, ambapo mapato ya malipo ya bima yameongezeka kwa asilimia 7.4, kutoka trilioni 1.15 mwaka 2022 hadi trilioni 1.24 mwaka 2023.

Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) inaendelea kuimarisha mahusiano na mazingira rafiki kwa watoa huduma za bima.

Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na TIRA, usajili wa bima umeongezeka kwa asilimia 30.4, kutoka shilingi bilioni 201.3 hadi bilioni 262.5.

Mwenyekiti wa Bodi ya Jubilee Life Insurance, Amyn Lalji, alihimiza sekta ya bima kuendelea kubuni bidhaa bunifu zinazoendana na hali halisi ya kifedha, akisisitiza kuwa bidhaa kama Akiba Flex ni muhimu kuwawezesha wananchi kupanga maisha yao ya baadaye kwa ufanisi na uendelevu.

Jubilee Life Insurance inaendelea kujikita katika kukuza ujumuishaji wa kifedha na ubunifu katika sekta ya bima ya Tanzania. Kupitia AkibaFlex, kampuni hiyo inaweka viwango vipya vya suluhisho linalomjali mteja, likiwasaidia Watanzania wengi zaidi kulinda maisha yao ya baadaye huku wakijenga utajiri. Uzinduzi huu unathibitisha dhamira ya Jubilee ya kuwawezesha wananchi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Bima ya Maisha ya Jubilee Helena Mzena, (Kulia). Kushoto ni Mkurugenzi mtendaji wa Jubilee Health Insurance Tanzania, Dr Harold Adamson, katika uzinduzi rasmi wa Mpango wa Akiba Flex.