Serikali yaonya wanaojipanga kuvuruga Uchaguzi Mkuu 2025

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 07:03 PM May 21 2025
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Innocent Bashungwa.
Picha: Mtandao
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Innocent Bashungwa.

Serikali imesema imejipanga kuhakikisha kuwa uchaguzi mkuu mwaka huu unafanyika kwa amani na utulivu na kwa yeyote ambaye atajaribu kutaka kufanya fujo ama kuharibu tukio hilo atachukuliwa hatua haraka.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Innocent Bashungwa amesema hayo leo Mei 21, bungeni wakati akijibu swali la mbunge wa Malinyi Antipas Mgungusi aliyetaka kujua lini serikali itapeleka magari ya polisi wilaya ya malinyi ili yatumike kutoa huduma kwa wananchi.

“Nitumie fursa hii kuwaeleza wabunge kuwa serikali imepanga kugawa magari kwa maofisa upelelezi wa jeshi la polisi nchini kote nchini kuanzia mwenzi Agosti mwaka huu.

“Na kuwa katika uchaguzi mkuu mwaka huu tumejipanga kwa namna zote ikiwamo vifaa kuhakikisha kuwa uchaguzi unafanyika kwa amani na utulivu na kwa yeyote atakayetaka kuharibu zoezi hili atachukuliwa hatua kali,”amesema Bashungwa

Kuhusu swali la mbunge amesema mwezi Septemba, 2023 serikali kupitia Jeshi la Polisi iligawa gari moja jipya lenye Namba za usajili PT 4851 Toyota Land Cruiser Pickup kwa Wilaya ya Malinyi, hivyo, kufanya wilaya hiyo kuwa na magari mawili ya Polisi yanayofanya kazi.

Aidha, serikali inaendelea kutenga fedha toka kwenye bajeti yake kila mwaka wa fedha kwa ajili ya ununuzi vitendea kazi mbalimbali yakiwemo magari na kuyagawa kwenye mikoa na wilaya zote hapa nchini.