Cherehani ashauri zao la embe kuingizwa kwenye ushirika

By Shaban Njia , Nipashe
Published at 06:07 PM May 21 2025
Mbunge wa Ushetu mkoani Shinyanga, Emmanuel Cherehani.
Picha: Mtandao
Mbunge wa Ushetu mkoani Shinyanga, Emmanuel Cherehani.

Mbunge wa Ushetu mkoani Shinyanga, Emmanuel Cherehani ameishauri Wizara ya Kilimo kuandaa utaratibu mzuri wa kulikomboa zao la embe kwa kuliingiza katika Ushirika ili kuchangia ukuaji wa mapato katika halmashauri mbalimbali hapa nchini zinazolima zao hilo.

Cherehani ameyabainisha haya leo wakati akichangia katika madirio ya Bajeti ya Wizara ya Kilimo ya mwaka wa fedha 2025/2026 iliyowasilishwa na Waziri Husein Bashe nakusema, zao hili limesahaulika kuliko mazao mengine na vijijini kuna magari yanapishana yakitafuta embe. 

Amesema, embe ni zao lenye tija na faida katika kuchochea uchumi lakini limesahaulika kutokana na kukosekana kwa utaratibu wa kuthaminiwa na mti mmoja unanunuliwa kwa Sh.2000 na ungekuwa unajaliwa ungenunuliwa kwa gharama kubwa na serikali ikapata mapato yake.

 “Tuliingize zao hili kwenye vyama vya ushirika ili yavunwe kwa utaratibu unaotakiwa na yatachangia mapato makubwa kwenye halmashauri zetu kama mazao mengine, leo yanavunwa kwa utaratibu usio mzuri kwani mti unatikiswa na yanaanguka mpaka machanga” ameongeza

 Wakati huo huo; Cherehani ameshauri wizara kuruhusu kuanzishwa soko la tumbaku kwa mfumo wa mnada ili kumpa mkulima uanda mpana wa kuuza tumbuku kwa bei itakayompatia faida na kumkomboa kiuchumi kuliko ilivyo hivi sasa wanavyopangiwa bei.