Chama cha ACT-Wazalendo Mkoa wa Shinyanga kimeanza rasmi mchakato wa ndani wa kupokea watiania wa kugombea nafasi ya ubunge katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, ambapo watiania nane wamechukua na kurejesha fomu za kugombea.
Kwa mujibu wa Afisa wa Organizesheni na Mafunzo wa Uchaguzi kutoka ACT-Wazalendo Taifa, Risasi Semasaba,amesema zoezi hilo limeanza leo Mei 21,2025, kwa majimbo ya Shinyanga Mjini, Kishapu, Solwa na Jimbo jipya la Itwangi, huku majimbo ya Kahama yakitarajiwa kufuatia.
Semasaba amebainisha kuwa, hadi sasa watiania wanane wamejitokeza kuchuka fomu hizo,na kwamba zoezi la uchukuaji wa fomu litaendelea hadi Mei 31, 2025, likifuatiwa na kura za maoni za chama ili kumpata mgombea mmoja kwa kila jimbo.
“Katika Jimbo la Shinyanga Mjini, waliotia nia ni Siri Yasini, Melkyoli Sebastian, Justa Denis, Simon Tungu na Mbaruku Haji, Jimbo la Kishapu lina mtiania Yakob Madoshi, Itwangi lina Hassan Ibrahimu, huku Jimbo la Solwa likiwakilishwa na Machanga Machanga,”amesema Semasaba.
Nao watiania wa nafasi hizo za ubunge akiwamo Siri Yasini, amesema kuwa endapo akipata ridhaa ya kuwa Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini,kwamba ataanza na vipaumbele vya kuboresha miundombinu mbalimbali ikiwamo ya barabara,ujenzi wa masoko, stendi za mabasi, na huduma za afya.
Amesema kuwa,Shinyanga ni Mkoa ambao una rasilimali nyingi yakiwamo madini,na ni Mkoa wa tatu kwa uchangiaji wa pato la taifa, lakini upo nyuma kimaendeleo,kuwa akipata ridhaa ya kuwa Mbunge, lazima ahakikishe rasilimali hizo zinachangiza maendeleo ya Mkoa huo.
Mtiania mwingine Hassan Ibrahimu kutoka Jimbo la Itwangi, amesema kwamba Jimbo hilo ni jipya, hivyo akipata ridhaa ya kuwa Mbunge, atahakikisha maendeleo yanapatikana kwa ustawi wa maisha ya wananchi, na kwamba muda wote atakuwa Jimbo kwa ajili ya kusikiliza kero za wananchi na kuzitatua.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED