BUNGE la Uganda limepitisha miswaada miwili tata inayodaiwa kulenga kudhoofisha vyama vya siasa na kwa ujumla upinzani nchini humo, ikielezwa kuwa wabunge wa upinzani waliondoka bungeni wakati miswaada hiyo ikipitishwa.
Imeelezwa kuwa Uganda imeingia katika njiapanda nyengine ya kidemokrasia, utawala wa kisheria na haki za binadamu baada ya kupitishwa kwa miswaada hiyo ambayo imeharakishwa sana ikilinganishwa na mingine.
Pia imeelezwa kuwa idadi kubwa ya wabunge wa upinzani waliondoka kwenye kikao asubuhi ya leo wakipinga kuendelea kwa mchakato huo bila kuruhusu muda wa kutosha kwa umma na wadau mbalimbali kutoa maoni yao kama inavyostahili kwa miswaada nyeti inayogusia demokrasia na utawala wa kisheria.
Imeelezwa kuwa hatua hiyo haikuzuia bunge hilo ambayo zaidi ya theluthi ya wabunge ni wale wa chama tawala cha NRM kuendelea na shughuli ya kujadili na kuipitisha miswaada hiyo.
Kiongozi wa upinzani bungeni, Joel Senyonyi aliyeongoza wenzake kususia kikao amesema kuwa watawasilisha kesi mahakamani kupinga kupitishwa kwa miswaada huo.
Imebainishwa kuwa muswaada wa kwanza kupitishwa ni ule ambao umelenga kukosesha vyama visivyojumuika katika kundi la pamoja la vyama vya siasa maarufu kama IPOD kutofadhiliwa na serikali.
Awali, vyama vilifadhiliwa kutokana na idadi ya wabunge wao na kwa hiyo chama cha NUP kinachoongozwa na Robert Kyagulanyi almaarufu Bobi Wine kimekuwa kikipata kiasi kikubwa cha fedha ambacho kama njia ya kudhihirisha uwazi na uwajibikaji kwa wafuasi wake kimejenga makao makuu katika kipindi kidogo cha miaka mitatu tu ikilinganishwa na chama tawala cha NRM ambacho hukodi.
Imeelezwa kuwa kupitishwa kwa muswaada tata zaidi ambao utarejesha mamlaka ya mahakama ya jeshi kuendesha kesi dhidi ya raia ndilo jambo ambalo limetumbukiza hali ya haki za binadamu Uganda katika mashaka zaidi.
Mamlaka hiyo ilifutiliwa mbali na mahakama ya juu ya rufaa mwezi Januari mwaka huu na kuwezesha kesi kadhaa za kisiasa ikiwemo ile ya uhaini dhidi ya kiongozi maarufu wa upinzani Dk. Kizza Besigye kuhamishwa hadi mahakama ya kiraia.
Kwa pamoja wabunge wa chama tawala wameahidi kuupitisha muswaada huo na wamecheleweshwa tu na mawasilisho ya wabunge wachache wa upinzani waliobaki wakati wenzao walipoondoka.
Imeelezwa kuwa jambo la kushtusha kuhusu muswaada huo wa kurejesha mamlaka ya jeshi juu ya raia ni kwamba raia akikamatwa kwa madai na vyombo vya jeshi atapewa cheo kwenye jeshi.
Imeelezwa kuwa cheo hicho kitatokana na kiwango cha uhusika wake katika kuvunja kanuni za kijeshi kama vile kupatikana na silaha au madai ya uhaini. Ni kwa njia hiyo, mahakama ya jeshi itamhukumu kama mmoja wao na sio raia.
Chanzo" DW
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED