Kambi maalum ya bure ya uchunguzi wa magonjwa ya moyo iliyoandaliwa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) katika kampasi ya Mloganzila imepokelewa kwa mwitikio mkubwa kutoka kwa wananchi wa jiji la Dar es Salaam, huku wengi wakielezea kufurahishwa na huduma walizopata.
Kambi hiyo ya siku mbili, iliyofanyika kama sehemu ya maandalizi ya uzinduzi wa awamu ya pili ya Kituo cha Umahiri cha Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa huduma za moyo, imelenga kuzuia na kugundua mapema magonjwa ya moyo kwa watu wa rika mbalimbali.
Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. Appolinary Kamuhabwa, amesema kambi hiyo ni miongoni mwa mikakati ya MUHAS katika kuhamasisha uchunguzi wa mara kwa mara wa moyo ili kudhibiti madhara ya kiafya yanayotokana na kutotambua matatizo ya moyo mapema.
“Uchunguzi huu unatoa nafasi kwa watu wengi kugundua hali zao za moyo kabla ya kuwa katika hatua mbaya. Tunaamini hii ni njia bora ya kuokoa maisha kwa gharama nafuu,” ameeleza Prof. Kamuhabwa.
Wananchi waliojitokeza kwa wingi kupima afya zao waliupongeza mpango huo, wakisema umewasaidia kupata huduma muhimu ambazo wengi wao huchukulia kuwa za gharama kubwa au ngumu kufikiwa.
Mtemi Chitema Mahunguchira, mkazi wa Mbagala, amesema:
“Nashukuru sana MUHAS kwa kuleta huduma hii karibu na wananchi. Wengi wetu hatujawahi kupima moyo kutokana na ukosefu wa elimu au hofu ya gharama. Hii ni hatua nzuri sana. Naomba programu kama hizi ziwe zinafanyika hata katika vituo vya afya vya wilaya.”
Naye Maria Thadeus, mkazi wa Mbezi, amethibitisha kuridhishwa na huduma aliyoipata katika kambi hiyo:
“Nilihudumiwa kwa haraka na kwa uangalifu mkubwa. Madaktari walinieleza hali yangu na kunishauri cha kufanya. Kwa kweli nimefarijika sana na nina matumaini ya kuanza mazoezi sahihi kulingana na ushauri wao.”
Kwa upande wa wataalamu, Irine Mzokolo, mtaalamu wa fiziolojia na msaidizi wa ufundishaji MUHAS, amesema kuwa huduma hiyo iliwalenga pia watu wenye hali za kiafya maalum, na kuwaelekeza juu ya umuhimu wa kuanza mazoezi kwa mpango ulioandaliwa kulingana na afya ya mtu.
“Tunaelekeza watu namna ya kufanya mazoezi salama. Wengi wamekuwa wakifanya mazoezi bila kujua hali zao za moyo, jambo ambalo linaweza kuwaletea madhara. Kupitia mpango huu, tunawawezesha kuanza safari ya afya kwa usalama,” amesema. 1