Makalla aeleza wananchi faida miradi inayotekelezwa na Rais

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 12:06 PM May 22 2025
Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM, CPA Amos Makalla.
Picha: Mpigapicha Wetu
Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM, CPA Amos Makalla.

Katibu wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM, CPA Amos Makalla, amewaeleza wananchi faida ya utekelezaji wa miradi mikubwa anayofanya Rais Samia Suluhu Hassan likiwamo bwawa la Mwalimu Nyerere, daraja la Kigongo-Busisi na Reli ya Kisasa (SGR), akisema imefungua fursa ya uchumi wa nchi na wa Watanzania.

Amesema miradi hiyo na mingine inayoendelea kutekelezwa pia, inarahisisha ufanyaji biashara kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine na kuunganisha wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi.

Amesema ndio maana anaingia katika rekodi ya marais waliopeleka fedha nyingi za maendeleo kutekeleza miradi maeneo mbalimbali nchini.

Makalla ameyasema hayo Mei 21, 2025, wakati akizungumza na wananchi katika maeneo tofauti Buchosa, Sengerema na baadae katika mkutano wa hadhara uliofanyika wilayani Misungwi, mkoani Mwanza.

Amesema daraja la Kigongo-Busisi limelenga  kufungua uchumi wa mikoa ya Kanda ya Ziwa, na kuwezesha biashara kufanyika.

“Tunaposema wanufaika wakubwa ni Wilaya ya Sengerema, maana yake Geita, Bukoba na Kigoma, lazima wapite Sengerema ili kupita darajani hapo. Uwapo wake lina manufaa makubwa kiuchumi ni daraja la tano kwa urefu Afrika,” amesema Makalla.

Amesema Rais Samia aliahidi atamalizia miradi yote likiwamo daraja hilo na kuwataka wananchi wampongeze kwa kuwa amefanya kwa vitendo.

“Tulikuwa na ujenzi wa meli kubwa ya kutoka Mwanza, Bukoba hadi Uganda, Rais Samia ameikamilisha..niliacha vivuko vinne vinatekelezwa na wabunge wenu walikuwa wanafuatilia nadhani viko hatua ya mwisho kukaamilika. 

“Daraja hili litatuunganisha si tu wilaya kwa wilaya, mkoa kwa mkoa litatuunganisha na nchi za nje na sisi tutanufaika na biashara,” amesema.

Amesema Rais Samia amekamilisha ujenzi wa SGR ulioachwa na mtangulizi wake Rais wa awamu ya tano, Hayati John Magufuli, na sasa anaendeleza kipande cha Dodoma hadi Mwanza.

Kadhalika, amesema Rais Samia amekamilisha pia, ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere ambalo limesaidia upatikanaji wa umeme wa uhakika.