Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, ametoa zawadi maalum kwa timu ya Simba kwa kugharamia matumizi ya Uwanja wa New Amaan Complex uliopo Unguja, utakaotumika kwa mechi ya fainali ya pili ya Kombe la Shirikisho la Afrika, itakayofanyika Jumapili, Mei 25, 2025 kuanzia saa 10 jioni dhidi ya RS Berkane .
Taarifa hiyo imetolewa kwa umma na Naibu Mkurugenzi wa Mawasiliano, Ikulu Zanzibar, ambapo imeelezwa kuwa uamuzi huo wa Dk. Mwinyi unadhihirisha mapenzi yake ya dhati katika michezo pamoja na kuhamasisha ushindi kwa Simba SC katika mechi hiyo ya kihistoria dhidi ya RS Berkane kutoka Morocco.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar za kuunga mkono maendeleo ya michezo na kuimarisha hadhi ya kimataifa ya visiwa vya Zanzibar katika nyanja za kimichezo.
Mbali na kuruhusu matumizi ya uwanja huo bila malipo, Rais Mwinyi pia amechukua jukumu la kugharamia maandalizi yote muhimu ya uwanja kwa ajili ya mechi hiyo ya fainali.
Aidha, fainali hiyo inatarajiwa kuhudhuriwa na maelfu ya mashabiki kutoka ndani na nje ya nchi, jambo linaloonyesha uzito wa tukio hilo kwa taifa.
Kwa kutambua umuhimu wa mechi hiyo kwa Tanzania, Rais Mwinyi ameahidi kuhudhuria fainali hiyo sambamba na Watanzania wengine wote katika kuwaunga mkono Simba SC na kuhamasisha ushindi wa kihistoria.
Timu ya Simba imefika hatua ya fainali ya michuano hiyo ya CAF baada ya kuifunga Stellenbosch ya Afrika Kusini kwa bao 1-0, na katika mechi ya kwanza ya fainali, ilipoteza ugenini mjini Berkane, Morocco kwa mabao 2-0. Hivyo basi, Jumapili hii, Simba itakabiliwa na kibarua cha kushinda kwa angalau mabao 3-0 ili kutwaa taji hilo kwa mara ya kwanza katika historia yake.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED