Rais wa zamani wa Jamhuri ya Afrika Kusini, Thabo Mbeki, amewasili mkoani Morogoro kwa ziara maalum ya kutembelea eneo la kihistoria la Mazimbu, ambalo lilikuwa makazi ya wapigania uhuru wa Afrika Kusini waliokuwa uhamishoni wakati wa utawala wa ubaguzi wa rangi.
Mbeki amesafiri kwa kutumia Treni ya Kisasa ya SGR kuelekea Morogoro kwa ajili ya kutembelea eneo hilo lenye historia ya kipekee.
Katika Stesheni ya SGR ya Jakaya Kikwete, Morogoro, Mbeki alipokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Adam Malima, pamoja na viongozi wengine wa Serikali.
Ziara hiyo ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Afrika yanayoadhimishwa kila mwaka tarehe 25 Mei, kama kumbukumbu ya kuanzishwa kwa Umoja wa Afrika (zamani ukijulikana kama OAU), pamoja na kuhamasisha mshikamano, maendeleo na utambulisho wa bara la Afrika.
Thabo Mbeki yupo nchini kwa mwaliko wa Taasisi ya Thabo Mbeki kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za hapa Tanzania, ambapo kwa pamoja wameandaa maadhimisho haya ya kitaifa ya Siku ya Afrika.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED