Mtanzania Faith Kapillima ameandika historia kwa kuchaguliwa kuwa Diwani wa Kata ya Victoria, nchini Uingereza kupitia chama cha Kihafidhina (Conservative Party).
Akizungumza na EATV baada ya ushindi huo, Faith amesema siri ya mafanikio yake katika siasa ni kupigania ajenda ya afya ya akili, hususan katika mapambano dhidi ya changamoto zinazowakumba watoto wenye usonji (autism), hali ambayo pia imeathiri mtoto wake wa kwanza.
“Ilichukua miaka mitatu kupata msaada kutoka serikalini ili mwanangu wa kwanza aweze kupata huduma stahiki na kurudi katika hali ya kawaida. Baada ya hapo, nikaona ni vyema nijiunge katika siasa ili nipate nafasi ya kusaidia familia nyingine zenye changamoto kama yangu,” amesema Faith.
Ameeleza kuwa kipaumbele chake kama Diwani ni kuhakikisha anawasilisha maoni ya wananchi katika mamlaka husika na kuboresha huduma za afya kwa watu wenye ulemavu, hasa kupitia mfumo wa huduma rafiki unaojali mahitaji yao.
“Tutaboresha huduma muhimu kama barabara, hospitali na pia kuhakikisha jamii inajumuishwa katika shughuli mbalimbali za kijamii ili kujenga mshikamano na ushirikishwaji,” amesisitiza Faith.
Pamoja na kuwa raia wa Tanzania aliyechaguliwa katika nafasi ya uongozi nje ya nchi, Faith amesema hajawahi kukumbana na ubaguzi wa aina yoyote nchini Uingereza, jambo ambalo linaonyesha jinsi jamii hiyo inavyothamini usawa na haki za binadamu.
Aidha, amebainisha kuwa ana ndoto ya kurejea nyumbani Tanzania siku moja ili kuwapeleka watoto wake kusalimia ndugu na kuifahamu nchi yao ya asili.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED