Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) kimesema kipo tayari kuwapokea wanachama wapya kutoka vyama mbalimbali vya siasa, wakiwemo waliokuwa wanachama wa kundi la G55 lililojitenga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) hivi karibuni.
Makamu Mwenyekiti wa CHAUMMA Tanzania Bara, Kayumbo Kabutali, amesema chama hicho hakina pingamizi kwa yeyote anayetaka kujiunga nao, lakini amekanusha uvumi kuwa tayari wameanza kuwapokea wanachama waliotoka Chadema.
“Hakuna wanachadema tuliowapokea hadi sasa, isipokuwa tunaendelea kuhamasisha nchi nzima watu kujiunga na chama chetu,” alisema Kabutali katika mazungumzo maalum na Nipashe Digital.
Aliongeza kuwa wanaendelea na maandalizi kuelekea Juni 27, 2025, ambapo tutatangaza majina ya wagombea wetu wa Urais, Ubunge na Udiwani.
Hata hivyo, mmoja wa viongozi wa juu wa CHAUMMA ambaye hakutaka jina lake litajwe, alikanusha taarifa zinazozagaa mitandaoni kuwa tayari chama hicho kina mazungumzo ya kuwapokea wanachama kutoka Chadema.
“Sio kweli hatujafanya mazungumzo na mtu yeyote, lakini milango ipo wazi kama siku hiyo watakuja, uamuzi wa kuwapokea au kutowapokea utategemea hali ya siku husika,” alisema kiongozi huyo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED