UBALOZI wa China umesifu nafasi ya kihistoria ya Tanzania katika kuhimiza kupitishwa kwa Azimio Na. 2758 la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) mwaka 1971, ambalo lilirejesha kiti halali cha China katika Umoja wa Mataifa na kuimarisha msimamo wa "China moja" kama makubaliano ya kimataifa.
Akizungumza hivi karibuni jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliopewa jina la ‘Azimio la UNGA Na. 2758 Halitikisiki na Msimamo wa China Moja Lazima Uzingatiwe’, Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian, alisifu uungwaji mkono thabiti wa Tanzania kwa China katika majukwaa ya kimataifa.
“Tangu kuanzishwa kwake, Tanzania iliunga mkono kwa dhati kurejeshwa kwa China katika Umoja wa Mataifa,” alisema. “Hatutamsahau kamwe Balozi Dk Salim Ahmed Salim, aliyekuwa Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa wakati huo, ambaye alitoa hotuba yenye nguvu kuunga mkono uwakilishi halali wa China — akisisitiza kuwa robo ya watu wote duniani walikuwa hawawakilishwi.”
Balozi Chen alieleza kuwa wakati ambao Dk Salim alisimama na kushangilia kupitishwa kwa Azimio Na. 2758 ulikuwa na ishara ya kipekee kwa watu wa China.
“Ilikuwa ni ishara ya mshikamano wa Tanzania na China katika suala nyeti la mamlaka na ukamilifu wa ardhi ya taifa.”
Azimio la UNGA Na. 2758 lilitambua Jamhuri ya Watu wa China kuwa “mwakilishi pekee halali wa China katika Umoja wa Mataifa.”
“Azimio hili linaakisi makubaliano ya jumuiya ya kimataifa,” alisema. “Uungwaji mkono thabiti wa Tanzania ni wa kihistoria na wa thamani kubwa, na tunaisifu kwa kujitolea kwake kwa dhati katika kuunga mkono msimamo wa China moja.”
Balozi huyo pia alikumbusha kuwa mwaka 2025 utatimiza miaka 50 tangu kukamilika kwa Reli ya TAZARA, mradi wa kihistoria unaoashiria urafiki kati ya China na Tanzania.
“Maadhimisho haya ni ya maana sana kwa uhusiano kati ya nchi zetu,” alisema.
Aliongeza kuwa China iko tayari kuendeleza ushirikiano na Tanzania katika nyanja za kisiasa, kiuchumi na kitamaduni.
“Tunalenga kutekeleza makubaliano ya viongozi wakuu wa mataifa yetu, kuimarisha uaminifu wa pande zote na kujenga jumuiya ya karibu ya China na Tanzania yenye mustakabali wa pamoja.”
Akirejelea ziara ya kitaifa ya Rais Samia Suluhu Hassan mjini Beijing, Balozi Chen alisema mazungumzo ya ngazi ya juu yalithibitisha uhusiano wa kudumu wa kidiplomasia kati ya Tanzania na China. Katika mkutano wake na Rais Xi Jinping, China iliahidi kuiinua Tanzania kuwa mfano wa ushirikiano wa hali ya juu kati ya China na Afrika chini ya Mpango wa Ukanda wa Barabara (BRI).
Aliongeza kuwa Tanzania inaendelea kuongoza katika mahusiano ya China na Afrika, huku uwekezaji wa China ukizidi kuleta matokeo makubwa katika sekta mbalimbali.
Kama sehemu ya ushirikiano mpana wa China na Afrika, Rais Xi aliahidi msaada na mikopo nafuu ya zaidi ya dola bilioni 50 ndani ya miaka mitatu ijayo. Fedha hizo zinalenga kusaidia juhudi za kisasa za Afrika, hasa katika miundombinu na kilimo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED