Dk. Samia: Hatusemi kutoka ndotoni, tukisema tunatekeleza

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:16 PM Sep 25 2025
Dk. Samia: Hatusemi kutoka ndotoni, tukisema tunatekeleza

Mgombea urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Samia Suluhu Hassan amesema kila kinachoahidiwa kinatekelezwa na Serikali, ndio maana hivi sasa huduma za matibabu ya kibingwa zinapatikana ndani ya mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara.

Dk Samia amesema kwa ujumla mambo ya afya kusini yapo vizuri kutokana na kazi nzuri ya uboreshaji na ujenzi wa miundombinu ikiwemo hospitali za kisasa uliofanywa na Serikali anayoingoza, ambayo ikiahidi inatekeleza. 

Mgombea huyo ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania amesema hayo leo Alhamisi Septemba 25,2025 wakati akizungumza na wananchi wa Jimbo la Mchinga mkoani Lindi,katika mkutano wa hadhara wa kampeni zake za kusaka kura katika uchaguzi mkuu ujao.

Dk Samia amesema kasi ya kuboresha sekta ya afya itakuwa ile ile ndani ya miaka mitano ijayo, kwa maeneo yasiyopata vituo vya afya, vitajengwa, akitolea mfano katika wa Mkoa wa Lindi Serikali imefanya kazi kubwa kuboresha na kurahisisha huduma hizo.

“Kwa mkoa wa Lindi, tumejitahidi huduma zote za afya zikiwemo za kibingwa, zinapatikana hapa hapa kwa sababu kuna hospitali kubwa ya rufaa inayotoa huduma zote. Lakini yale matibabu makubwa wanaweza kwenda Muhimbili au maeneo mengine,”

“Lakini huduma nyingine za kibingwa zitapatikana hapa hapa (Lindi), kwa bahati nzuri jirani zenu wa Mtwara watapata huduma za kibingwa pia,” amesema Dkt Samia.

Septemba 22,2025 akiwa mkoani Ruvuma, Dk Samia alisema ujenzi wa hospitali ya mkoa huo upo mbioni kukamilika hatua itakayowezesha huduma za matibabu ya kibingwa kupatikana mkoani humo badala ya wananchi kwenda mikoa mingine.

“Hakuna chama kitakachoweza kulinda na kuinua utu wa Mtanzania, kama Chama Cha Mapinduzi, ndio maana tumekuja na kauli mbiu ya ‘Kazi na Utu, Tunasonga Mbele’. Tupeni ridhaa yenu CCM tuendesha nchi hii tena kwa miaka mitano ijayo, tufanye kazi ili kuinua utu wa Mtanzania,” ameeleza.

Katika mkutano huo, Dk Samia amewaahidi wananchi wa Mchinga kuboresha barabara ya Milola- Kiwawa na zingine zilizoanishwa katika ilani ya uchaguzi ya chama hicho tawala.

“Pamoja na hilo, tutajenga stendi ya malori hapa Mchinga ili kupunguza msongamano na kuongeza fursa ya biashara katika eneo hili,” amesema Dk.  Samia.