Fanyeni tafiti zenye tija kwa wananchi- Majaliwa

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:52 PM Jun 18 2025
Fanyeni tafiti zenye tija kwa wananchi- Majliwa

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ametoa wito kwa watafiti na wapangaji wa sera nchini kuwekeza katika tafiti zenye tija kwa wananchi, akisisitiza umuhimu wa kuyatumia matokeo ya tafiti hizo badala ya kuyaweka kwenye makabati.

Majaliwa amesema kufanya hivyo kutaiwezesha Serikali kuwa na matokeo yanayotumika kutengeneza sera na mipango ya utekelezaji yenye kuleta mabadiliko halisi katika jamii.

Ametoa wito huo leo, Jumatano Juni 18, 2025, kwenye Kongamano la 13 la Kisayansi la Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), lililofanyika katika Kampasi ya Mloganzila, jijini Dar es Salaam.

“Tunataka kuona matokeo ya tafiti hizi yanatumika, msiweke tafiti hizi kwenye makabati tu, matokeo haya yanapaswa kuleta tija katika sekta ya afya. Ni matarajio yangu kuwa kongamano hili litatumika kutoa mapendekezo yatakayoimarisha mifumo, sera, na ushirikiano baina ya sekta ya umma na binafsi ili kuhakikisha Watanzania wananufaika kikamilifu na mapinduzi haya,” amesema Majaliwa.

Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka wadau wa sekta binafsi na washirika wa maendeleo kuongeza uwekezaji katika vifaa tiba na teknolojia mpya ili kuongeza uwezo wa Taifa kukabiliana na magonjwa kwa wakati.

Amesema Serikali itaendelea kuboresha sekta ya afya kwa kuwekeza zaidi katika miundombinu, rasilimali watu, tiba za kibingwa na mifumo ya kukabiliana na milipuko ya magonjwa.

“Tutaendelea kushirikiana na wadau wote kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma bora, salama na rafiki bila kujali mahali alipo,” ameongeza Majaliwa.
1

Pia amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuweka mazingira wezeshi ya kuvutia uwekezaji katika uzalishaji wa dawa, chanjo na vifaa tiba nchini. “Tayari tumeanza kushuhudia hatua chanya katika maeneo haya, tukijivunia mchango wa wataalamu wetu wa ndani,” alisema.

Aidha, amesema Serikali imeendelea kuimarisha matumizi ya teknolojia katika sekta ya afya ambapo kwa sasa hospitali nyingi zinatumia mifumo ya kidijitali kubaini magonjwa, kutoa tiba sahihi na kufuatilia maendeleo ya wagonjwa.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu (Sayansi, Teknolojia na Elimu ya Juu) kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Daniel Mushi, amesema Serikali imeweka kipaumbele kikubwa katika elimu, sayansi na teknolojia ili kuimarisha maendeleo ya Taifa.

“Tunajivunia mageuzi makubwa chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, uongozi wake umeleta mageuzi mapya katika kuimarisha taasisi za elimu nchini,” alisema Prof. Mushi na kuongeza kuwa maboresho yaliyofanyika katika Chuo hicho ni ushahidi wa dhamira ya Serikali kuboresha mazingira ya ujifunzaji na ufundishaji.
2

Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu hicho, Prof. Appolinary Kamuhabwa, ameipongeza Serikali kwa jitihada za dhati ambazo zimewezesha kupatikana kwa ushirikiano mkubwa kutoka kwa wadau mbalimbali wa maendeleo, hali iliyopelekea utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati inayolenga kuboresha elimu ya juu na huduma za afya nchini.

Prof. Kamuhabwa ametaja miongoni mwa miradi hiyo kuwa ni ujenzi wa Kituo cha Umahiri cha Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu cha Afrika Mashariki (East African Centre of Excellence for Cardiovascular Sciences), unaofadhiliwa na Serikali kupitia mkopo wa masharti nafuu kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).

Amesema mradi huo kwa sasa umeingia awamu ya pili baada ya kukamilika kwa awamu ya kwanza ambayo iligharimu Shilingi bilioni 21.62. “Awamu ya pili ya mradi huu, ambayo ilianza rasmi mwezi Mei 2025, inalenga kujenga hospitali ya kisasa ya kufundishia wataalamu bingwa wa magonjwa ya moyo na mishipa ya damu,” alisema Prof. Kamuhabwa.

Amebainisha kuwa hospitali hiyo itaimarisha uwezo wa kutoa huduma za kibingwa, kufundisha wataalamu wa ndani na nje ya nchi, pamoja na kufanya tafiti zitakazosaidia kukabiliana na changamoto za magonjwa ya moyo na mishipa ya damu. “Awamu hii itagharimu kiasi cha Shilingi bilioni 221.57,” ameongeza.

3