UAMUZI uliofanywa na serikali mwaka 2020 kwamba Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ikusanye mapato yatokanayo na utalii, umesababisha miradi mikuu ya utalii na uhifadhi nchini kukwama.
Kupitia Sheria ya Fedha ya Mwaka 2020, serikali iliagiza mapato ya utalii yakusanywe na TRA kuanzia Julai Mosi 2020, huku ikiahidi ndiyo itakuwa inatoa fedha zinazohitajika kwa maendeleo ya hifadhi hizo.
Kabla ya uamuzi huo, mapato hayo yalikusanywa na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA), Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA). Mamlaka hizo ziliyakusanya na kutumia sehemu ya mapato hayo kwa shughuli za utalii na uhifadhi.
Baada ya TRA kupewa jukumu, sheria inaelekeza mamlaka hizo kuomba fedha Serikali Kuu kwa ajili ya mishahara ya watumishi, miradi ya maendeleo na matumizi mengine (OC).
Uamuzi huo, kama ilivyoelezwa bungeni Juni 2020 na aliyekuwa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango – sasa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anayejiandaa kustaafu baadaye mwaka huu, ulilenga kuongeza ufanisi katika makusanyo na kudhibiti matumizi ya mapato ya utalii nchini.
Hata hivyo, wakati wa mjadala wa Muswada wa Sheria ya Fedha ya Mwaka 2020, uamuzi huo wa serikali ulipingwa vikali na baadhi ya wabunge walioongozwa na aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT Wazalendo), Zitto Kabwe – mchumi aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC).
Hoja ya Zitto na wabunge wenzake ilikuwa kwamba serikali ina mwenendo usioridhisha katika utoaji fedha za miradi ya maendeleo, hivyo “uamuzi wa kupoka mapato ya TANAPA, NCAA na TAWA ni hatari kwa uendelevu wa utalii na uhifadhi nchini.”
Leo ikiwa imetimu miaka mitano ya bajeti tangu serikali itangaze hatua hiyo, madhara ya kutofanyiwa kazi angalizo la Zitto na wabunge wenzake yanaonekana dhahiri.
Imebainika serikali inatoa fedha pungufu na wakati mwingine kutotoa kabisa fedha za kutekeleza miradi ya hifadhi, hata kusababisha kuzorota kwa miundombinu inayosaidia huduma za utalii na hivyo kutishia ukuaji wa utalii na utoaji huduma.
“Kwa kweli katika miaka hii mitano tumepitia kipindi kigumu sana. Ukosefu wa fedha umesababisha tuwe na miundombinu duni hifadhini na kukwamisha mikakati yetu ya kuwadhibiti wananchi kuvamia maeneo ya hifadhi,” alisema mmoja wa maofisa waandamizi wa TANAPA katika mazungumzo na mwandishi jijini Arusha mwezi uliopita.
“TANAPA tuna majukumu mengi ikiwamo kukabiliana na kuota, kuenea na kusambaa kwa mimea vamizi na taka ngumu zinazozorotesha mfumo wa ikolojia wa hifadhi zetu. Yote haya yanahitaji fedha. Tuna matumaini mambo yatabadilika kutokana na serikali kuamua kuturejeshea walau asilimia 51 ya mapato yetu,” alieleza ofisa huyo.
Kwa mujibu wa ofisa huyo aliyeomba hifadhi ya jina lake, miradi mingi ya TANAPA inayojumuisha utafiti, ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya ndani na pembeni mwa hifadhi imekwama kutokana na ukosefu wa fedha.
Hoja hiyo ina uthibitisho katika ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ikiwamo ya mwaka 2020/21 inayobainisha kuwa katika mwaka huo wa kwanza wa utekelezaji uamuzi wa serikali, NCAA iliomba Sh. bilioni 31.21 kulingana na bajeti yake ya maendeleo, lakini serikali ilitoa Sh. bilioni 10.27 (asilimia 33).
Kutokana na upungufu wa fedha, CAG Charles Kichere anabainisha kuwa miradi 15 ilitekelezwa kati ya miradi 36 ya NCAA iliyoidhinishiwa fedha na Bunge. Fedha zilichelewa kutolewa kwa miezi saba. Mamlaka iliomba fedha hizo Oktoba 21, 2020, lakini serikali ilizitoa Mei 5, 2021 – siku 56 kabla ya mwaka wa fedha kufika ukomo.
Kwa upande wa TANAPA, bajeti ya maendeleo ya shirika kwa mwaka ilikuwa Sh. bilioni 69.52, lakini serikali ilitoa Sh. bilioni 26.51 sawa na asilimia 38 ya bajeti iliyoidhinishwa na Bunge. Hiyo ni 2020/21.
Ripoti ya CAG ya 2023/24, mwaka wa tano wa utekelezaji uamuzi huo wa serikali, inabainisha TANAPA iliidhinishiwa Sh. bilioni 23.036 kwa bajeti ya miundombinu ya hifadhi za taifa, lakini Sh. bilioni 21.97 (asilimia 95) hazikutolewa na serikali.
Vilevile, ripoti inabainisha Sh. bilioni 28.61 zilizoidhinishwa kwa ajili ya bajeti ya maendeleo ya NCAA, hazikutolewa na serikali licha ya TRA kukusanya Sh. bilioni 637.60 kwa niaba ya TANAPA na NCAA.
CAG Kichere ana angalizo kwamba: “Kutolewa fedha chini ya bajeti kunachangia kutotekelezwa miradi ya maendeleo. Hali hii ikiendelea, itasababisha kuzorota kwa miundombinu inayosaidia huduma za utalii, itaathiri ukuaji wa utalii na kutatiza utoaji huduma na hatimaye kupunguza mapato kwa serikali.”
Ripoti ya ukaguzi wa usimamizi na uendelezaji miundombinu ya TANAPA mwaka 2023/24 iliyotolewa na CAG Machi mwaka huu, inabainisha shirika lilipokea Sh. bilioni 1.060 kati ya Sh. bilioni 23.036 zilizoidhinishwa na Bunge kwa ajili ya kazi hiyo kwa mwaka tajwa.
“Ukosefu wa fedha za maendeleo ulisababisha kuchelewa kukamilika kwa miradi 15 ya maendeleo yenye thamani ya Sh. bilioni 14.12 inayotekelezwa na hifadhi 10 za taifa. Ucheleweshaji huo ulianzia miezi 10 hadi 33,” CAG Kichere anabainisha.
Vilevile, mapitio ya Mpango wa Mwaka 2023/24 wa Matengenezo ya Barabara, yamebaini hifadhi 12 za taifa zina mtandao wa barabara wa Km 25,683.9. Hifadhi hizo ni Serengeti, Katavi, Ziwa Manyara, Mikumi, Nyerere, Ruaha, Burigi, Arusha, Tarangire, Mkomazi, Saadani na ilimanjaro.
TANAPA ilipanga kufanya matengenezo ya Km 6,712.2 kati ya Km 25,683.9, lakini ilitengeneza Km 4,022; sawa na asilimia 60 ya lengo. Km 2,690.2 hazikutengenezwa kutokana na shirika kukosa fedha.
Kwa mwaka huo wa fedha, NCAA iliidhinishiwa na Bunge Sh. bilioni 28.61 kwa ajili ya bajeti ya maendeleo iliyojumuisha miradi minane, ikiwamo ya ujenzi wa vibanda vya walinzi na mageti ya kuingia na kutoka hifadhini, barabara na maji; lakini kiasi hicho hakikutolewa na serikali.
TIJA YA UHIFADHI
Yanayoendelea TANAPA na NCAA hivi sasa, yanaibua kumbukumbu za mwaka 1959. Mjerumani aitwaye Bernhard Grzimek, mwanaharakati wa uhifadhi wa asili, aliandika na kutengeneza filamu iitwayo Serengeti Shall Not Die – Serengeti Haitakufa.
Ujumbe wa filamu ulilenga kuitaka jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua za haraka kulinda na kuhifadhi Mbunga ya Serengeti na thamani yake kiikolojia “kwa manufaa ya wakazi wa eneo husika na jamii za kimataifa”.
Nani leo ataandika na kutengeneza filamu ya TANAPA na NCAA kuwa hazitakufa? Na mamlaka hizi ni kiburudisho kwa watu wa ndani na nje ya nchi, ni ajira, ni mali. Mwaka 2023/24 pekee, mamlaka hizi mbili ziliingizia serikali Sh. bilioni 637.60.
Unahitaji kujua kuwa TANAPA sasa inasimamia hifadhi 21 za taifa kutoka 22 zilizokuwapo kabla ya Juni 2023 Rais Samia Suluhu Hassan alipotangaza kufuta Hifadhi ya Taifa Kigosi kwa lengo la kuanzisha Msitu wa Hifadhi Kigosi ili kuwanufaisha kiuchumi wananchi wa mikoa mitano ya Geita, Kagera, Kigoma, Shinyanga na Tabora kwa kufuga nyuki na kuvua samaki.
NCAA ni msimamizi wa Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro, Pori la Akiba Poloreti na hifadhi ya kumbukumbu ya mambo ya kale ya Olduvai Gorge. Mamlaka hii inasimamia pia maeneo manne ya urithi wa kitamaduni, yaani Engaresero, Engaruka, Kimondo na Mapango ya Amboni ambayo ni miongoni mwa maeneo muhimu ya kiikolojia Afrika Mashariki.
Aidha, unahitaji kujua kwamba utalii ni uchumi. Juni 12 mwaka huu, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo aliarifu Bunge kuwa kwa mwaka 2024/25, vivutio vya utalii nchini, zikiwamo hifadhi za taifa, vilitembelewa na watalii 4,244,266. Kwa mwaka 2023/24 vilivuta watalii 3,784,214.
Vilevile, Mei 19 mwaka huu, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dk. Pindi Chana alisema bungeni kwamba Sekta ya Utalii sasa inachangia asilimia 17.2 katika Pato ghafi la Taifa na ina mchango wa asilimia 25 katika kuingiza fedha za kigeni nchini huku ikitoa ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kwa watu milioni 3.6 kwa mwaka.
Waziri Chana pia alitaja maeneo ya hifadhi ni vyanzo vikuu vya maji, nishati, makazi ya wanyamapori na viumbe hai wengine. Uendelevu wake unapaswa kupewa kipaumbele kibajeti.
Sera inaelekeza serikali kuongeza mchango wa utalii katika Pato la Taifa kwa kukuza na kuimarisha shughuli za kiutalii zinazojumuisha mawasiliano na uchukuzi.
Hali hii pia ni kinyume cha Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa Miaka Mitano (2021/22-2025/26), unaoelekeza uimarishaji vivutio vya utalii ili kuchangia katika Pato la Taifa na kutoa fursa za ajira.
Mpango unaelekeza ifikapo mwaka 2026, idadi ya watalii nchini iongezeke kutoka watalii 1,527,230 mwaka 2019/20 hadi milioni 5,000,000; na mapato ya utalii yafikie Dola za Marekani bilioni sita (6) kwa mwaka.
KAMATI YA BUNGE
Juni 19 mwaka huu, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Timotheo Mnzava alisema bungeni kuwa TANAPA na NCAA zimekumbwa na changamoto katika maeneo ya kutolea huduma za watalii na kushindwa kutekeleza shughuli za uhifadhi kwa ufanisi.
“Hali hii imechangia watalii wengi nchini kushindwa kufika katika vivutio vingi kwa wakati. Kamati inaitaka serikali kurejesha utaratibu wa TANAPA na NCAA kukusanya na kutumia (mapato yao) ili kuwezesha mamlaka hizi kujiendesha kwa ufanisi,” alisema.
Ni hoja iliyoungwa mkono na Mbunge wa Moshi Mjini, Priscus Tarimo ambaye alirejea Ripoti ya CAG ya mwaka 2023/24, akisema “Sh. bilioni 28 zilipaswa kutolewa na serikali kwa ajili ya kutekeleza miradi ya NCAA, lakini mamlaka hiyo iliambulia sifuri.”
Kwa upande wa TANAPA, mbunge huyo alisema “Serikali ilipaswa kutoa Sh. bilioni 23, lakini zilitolewa Sh. bilioni moja tu. Ng’ombe anayekamuliwa hachinjwi, bali analishwa vizuri. Fedha haziendi inavyotakiwa; mamlaka hizi zitakufa. Kuwapo barabara mbovu hifadhini, si tu kunatesa mtalii, bali hata magari ya wafanyabiashara yanaharibika.”
Mbunge wa Viti Maalum, Cecilia Pareso alisema fedha za utalii kukusanywa na TRA kisha kupelekwa Mfuko Mkuu wa Serikali, kumesababisha mamlaka za uhifadhi na shughuli za utalii kupitia alichoita “kipindi kigumu”.
“Kuomba fedha serikalini ni mchakato mrefu. Wabunge tumeishauri serikali iachie fedha kiasi zikasaidie maendeleo ya uhifadhi na utalii,” Cecilia alisema.
HATUA SERIKALINI
Juni 25 mwaka huu wakati wa mjadala wa Muswada wa Sheria ya Fedha ya Mwaka 2025, Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba alitangaza uamuzi mpya kuhusu mapato yatokanayo na utalii.
Alisema serikali imeamua kufanyia marekebisho Sheria ya Hifadhi za Taifa [Sura 282], Kifungu cha 9. Sheria mpya inaweka mgawanyo wa asilimia 91 ya mapato yatokanayo na huduma zinazotolewa na TANAPA. Asilimia 51 itawekwa katika akaunti ya taasisi hiyo iliyoko Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na asilimia 40 itapelekwa Mfuko Mkuu wa Serikali.
Hata hivyo, sheria mpya inaweka sharti la mamlaka kuomba kibali kutoka kwa Mlipaji Mkuu wa Serikali kabla ya matumizi ya fedha zinazowekwa katika akaunti ya TANAPA.
Kuhusu NCAA, Dk. Mwigulu alisema serikali imeamua kufanyia marekebisho Sheria ya Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro [Sura 284], Kifungu cha 12. Sheria mpya inaweka mgawanyo wa asilimia 91 ya mapato yatonakayo na huduma zinazotolewa na NCAA, ambapo asilimia 51 itawekwa katika akaunti ya mamlaka iliyoko BoT na asilimia 40 itapelekwa Mfuko Mkuu wa Serikali.
Kama ilivyo kwa TANAPA, sheria mpya inaweka sharti la mamlaka kuomba kibali kutoka kwa Mlipaji Mkuu wa Serikali kabla ya matumizi ya fedha zinazowekwa katika akaunti yake.
Chacha Nyandongo, Mwongoza Watalii wa Kampuni, Ndoto Kubwa Tours & Safaris ya jijini Arusha, anakosoa sharti la kuomba kibali cha matumizi ya fedha kutoka kwa Mlipaji Mkuu wa Serikali kabla ya matumizi ya fedha walizoidhinishiwa. Amefafanua:
“Hata ukiwasilisha andiko bora kiasi gani, utoaji fedha utabaki kuwa utashi wa Mlipaji Mkuu wa Serikali. Je, mlipaji ana uelewa wa kina kuhusu masuala ya utalii na uhifadhi? Hapa ninaona bado pana tatizo. TAWA, TANAPA na NCAA wataomba fedha lakini hawatapewa kwa wakati au watapewa fedha pungufu.
“Tuepuke kuingiza siasa katika utalii na uhifadhi. Miundombinu ya hifadhi zetu ni mibovu. Maeneo ya hifadhi ni makubwa na yako mbali na maeneo ya mijini. Unahitaji uwe na miundombinu mizuri hifadhini ili uwafanye wageni wako wafurahie safari,” ameeleza Chacha na kuongeza:
“Sasa fikiria barabara zetu zina mashimo, hazipitiki majira yote ya mwaka, mvua kidogo tu ikinyesha magari yanakwama, yanazama katika tope na mengine yanapinduka yakiwa na wageni, yanaharibika na kuhitaji bajeti kubwa ya matengenezo.”
Chacha anayejitambulisha ana uzoefu wa miaka 22 akiwaongoza watalii wanaotembelea NCAA na Hifadhi za Taifa za Serengeti, Arusha, Kilimanjaro, Tarangire na Ziwa Manyara, anatoa angalizo kwamba “mtalii akishapinduka na gari hifadhini na kuumia, usitegemee ataisema vyema Tanzania akirejea kwao”.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Oran Njeza anasema wamepokea uamuzi huo na kuishauri serikali ifanye uchambuzi zaidi kwa kuwa kamati imebaini asilimia 51 ya mapato ya TANAPA iliyopangwa kurejeshwa, haitoshi kuendeleza miundombinu ya utalii.
“Sheria ya Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro [Sura 284] imefanyiwa marekebisho katika kifungu cha 12 kwa lengo la kuweka mgawanyo wa mapato ya NCAA yanayokusanywa na TRA kama ifuatavyo:
“Asilimia tisa (9%) itawekwa katika akaunti maalum iliyofunguliwa BoT. Asilimia tatu (3%) ya kiwango hicho, itakuwa kwa ajili ya Mfuko wa Hifadhi ya Wanyamapori Tanzania na asilimia sita (6%) itakuwa kwa ajili ya Tozo ya Maendeleo ya Utalii.
“Asilimia 51 (ya mgawanyo wa asilimia 91), itawekwa katika akaunti ya NCAA iliyofunguliwa BoT na asilimia 40 itawekwa katika Mfuko Mkuu wa Serikali,” Mwenyekiti Njeza anasema.
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Waongoza Utalii Tanzania (TATO), Elirehema Maturo, anasema wanaamini uamuzi mpya wa serikali utasaidia kuboresha miundombinu ya hifadhi na shughuli za utalii ambazo zinahitaji fedha.
“Serikali inapaswa kuangalia mamlaka hizi kwa jicho la kipekee na kuzipa fedha za kutosha ili kuziwezesha kujiendesha. Wito wetu TATO ni kwamba fedha za utalii zitumike kama inavyotarajiwa,” anasema.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED