Heche: Zuio la siasa halitaiua CHADEMA

By Enock Charles , Nipashe
Published at 03:59 PM Jun 21 2025
Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA bara, John Heche
PICHA: MTANDAO
Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA bara, John Heche

Ikiwa imepita wiki moja tangu Mahakama kuweka zuio la kisiasa kwa Chama cha Demokraisa na Maendeleo (CHADEMA) chama hicho sasa kitaelekeza nguvu katika shughuli za kijamii ili kuendelea na kampeni yake ya 'no reforms no election'.Makamu Mwenyekiti wa chama hicho bara, John Heche pia amesema yafuatayo

Swali: Kuna zuio la kisiasa CHADEMA inafanya nini ili kuendelea na programu zake mbalimbali?

Heche: Hata likiendelea miaka 20 halitukatishi tamaa halituondoi kwenye msimamo wanachama wetu wapo tayari , viongozi wapo tayari , mapambano tumeanzisha na tutashinda, ANC ilifutwa na dola ya makaburu wakati ule kilikuwa na msimamo kama wa kwetu wa kutaka watu weusi waruhusiwe kupiga kura waonekane kama binadamu, viongozi wa ANC waliuwawa na akina Thabo Mbeki wakakimbia nje ya nchi lakini hawakufanikiwa kuzuia kiu ya wananchi ya kutaka mabadiliko kiu ya mabadiliko haiwezi kuzuiwa na zuio la mahakamani, wala na shambulio la kumuweka Lissu ndani, wanaodondoshwa madarakani na wananchi huwa hawajui kwamba watadondoshwa maana ungejua kwamba utadondoka kesho leo ungechukua hatua kujirekebisha , huwa wana kiburi, wakati nilipokuwa mbunge nilienda Sudani kipindi Omary Bashir akiwa Rais wa Sudani ungeniambia mimi kwamba wiki ijayo Omary Bashir angeondolewa madarakani ningekupinga sana kwasababu ni nchi ya kijeshi, kila mahali unakutana na wanajeshi wamesimama lakini maandamano yaliyoitishwa kwenye mitandao na akina mama baada ya hapo the rest is history alitolewa madarakani. 

Swali: Vipi kuhusu Zanzibar maana inadaiwa Sheria zake ni nafuu kwa uchaguzi? 

Heche: Hatuhitaji hisani ili tushinde uchaguzi tunahitaji mazingira mazuri ya kutenda haki sio kuonewa huruma ili tushinde kwahiyo ndio maana tunahitaji mabadiliko ya Kikatiba, kisheria na kiutaratibu kwa namna ya kuunda hizi tume za uchaguzi, namna ya kusimamia uchaguzi wa nchi hii, namna ya kufanya wananchi waamue nani awe kiongozi , kama Zanzibar kungekuwa na haki ya uchaguzi Maalim Seif angeshinda uchaguzi maana alishinda halafu Jecha akafuta uchaguzi yeye peke yake tume ikiwa hivihivi nani anawaambia leo kwamba yule bwana ambaye hana umaarufu kama wa Maalim Seif atashinda uchaguzi na kutangazwa? ni kujilisha upepo hakuna mwanasiasa amekuwa na nguvu kama Maalim Seif Zanzibar.

 Swali: Kukamatwa Lissu kumeleta athari gani katika chama?

Heche:Lissu ni kiongozi wetu mkubwa na ushawishi mkubwa kwenye nchi hii na hata waliomkamata walilenga kuathiri chama ni ukweli kwamba kama angelikuwepo mabo yasingelikuwa kama hivi yalivyo ni mtu ambae anaungwa mkono zaidi na wananchi, lakini ukweli ni kwamba wananchi wameona hilo na wametuunga mkono, kumshikilia Lissu kunaiumiza Serikali zaidi kuliko kuiumiza CHADEMA kitaifa na kimataifa kwa sababu kila mtu mwenye akili anajua ile ni kesi ya kisiasa dunia imezungumza, mashirika ya kimataifa yamezungumza, wanaharakati wamekuja hapa wakapigwa wakafanyiwa vitendo vya unyanyasaji, watu walikuwa hawajui mambo ya Tanzania, lakini sasa wamejua kwahiyo kuna athari kubwa kwa Serikali mpaka imelazimika kujibu huko UN na wamejaribu kudanganya lakini kila kitu kinajulikana, taswira ya Tanzania imeathirika kimataifa.

Swali: Je Chadema inasambaratika?

Heche: Kila mtu ana haki ya kuona vile anavyoona lakini ninachoweza kusema chama chetu ni taasisi kipo katika kila kitongoji cha nchi hii kuna ‘level’ ya kijiji CHADEMA tunaita tawi tuna kila kiongozi katika tawi la nchi hii, tuna viongozi kwenye Kata, CHADEMA ina viongozi kwenye kila Kata nchi hii, ina viongozi kwenye majimbo yote, ina viongozi kwenye Wilaya zote, ina viongozi kwenye mikoa yote, kwenye Kanda zote, tuna viongozi kwenye Kamati Kuu na tuna vikao vya kitaifa ambayo ni Baraza Kuu, Mkutano Mkuu na tuna kikao cha Kamati Kuu.

 Kwenye Baraza Kuu lenye watu zaidi ya 450 walioondoka mpaka sasa tunapozunguma na kwenda kwenye chama kingine ni watu 20 tu, na wameondoka katika wilaya zingine wameshajaza viongozi, kwahiyo nafasi ukiacha watu wengine wanakaa pale kwasababu CHADEMA ina watu wengi, kwenye Mkutano Mkuu walikuwa wameondoka watu chini ya 40 kati ya watu zaidi ya 1200 na tayari nafasi zao zimezibwa, kwenye Kamati Kuu ameondoka mjumbe mmoja kutokea Kanda ya Kati na kama isingekuwa haya mambo ya zuio la Mahakama tayari tulishatangaza uchaguzi kanda ya Kati na watu wanne wamejitokeza kugombea Kanda ya Kati kuja kuziba hiyo nafasi.

Kwahiyo hakuna ombwe kuonesha kwamba labda chama kina uhaba kuna upungufu au chama kinasambaratika hilo halipo kabisa, mashambulizi yanayotokea katika chama chetu yapo ‘coordinated’ kiserikali na ni kwa sababu kuna ‘impunity’ kwenye nchi hii na chama chetu kinataka serikali ifuate sheria ifuate utaratibu na serikali haitaki kufuata sheria kwahiyo inatumia mbinu nyingi kushambulia la kwanza wamemkamta Lissu na kumpa kesi ya uhaini, uhaini ni kesi kubwa ina viwango vyake huwezi kupanga uhaini wewe peke yako ‘as an individual’ ukapanga uhaini Lissu labda angekuwa na watu wamekutwa jeshini walikuwa nae wanapanga hayo mambo ya kupindua.

Swali: Unatathmini vipi kesi ya Lissu?  

Heche: Kesi yake ni ya uongo na tunaiona ni kama shambulio dhidi ya chama chetu kwasababu  uhaini ni nini? ni kumshambulia Rais labda ili kumdhuru, kumpindua, kumshambulia Spika kumuua au kumdhuru au Waziri Mkuu hivi sasa hayo mambo hayawezi kupangwa na mtu mmoja, shambulio la pili walimtumia mtu mmoja anaitwa Lembruce Mchome kikawaida wewe unapolalamika wewe ndiyo una burden ya kuprove Mchome alipoenda kulalamika aliandika barua kama rufaa sisi tukamwambia Msajili wewe sio mamlaka ya rufaa ya chama chetu, Msajili akaigeuza hiyo barua akasema ni barua ya malalamiko lakini unapolalamika wewe ndiyo unatakiwa kutoa uthibitisho ,sasa aliyelalamika hajathibitisha lakini Msajili amechukua hatua. Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA bara, John Heche

Shambulio la tatu ni haya yaliyoendelea Msajili kusema hatambui viongozi wetu, kufunga ruzuku ya chama, sheria inataka hoja inayoweza kusababisha ruzuku ikafungwa ni hoja moja tu kama CAG amekagua na kukuta labda tuna matumizi mabaya fedha, shambulio jingine ni hii kesi inayoendelea kuhusu mgawanyo wa mali sisi tulipoingia hatujawahi kubadilisha chochote au kufanya mgawo upya au kununua hata kiwembe kusema kwamba tugawanye sasa wale waliokuwa madarakani ndio wameenda Mahakamani kulalamika kuhusu mgawanyo wa mali kwahiyo haya yote ni kwa sababu ya msimamo wetu ambao tumechukua kwamba ‘no reforms no election’ kama hakuna mabadiliko tutahamasisha kwamba kusifanyike uchaguzi.