Kihenzile aipa kongole TCAA utekelezaji mradi wa mawasiliano

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 12:51 PM Jun 05 2025
Kihenzile aipa kongole TCAA utekelezaji mradi wa mawasiliano
PICHA: MAULID MMBAGA
Kihenzile aipa kongole TCAA utekelezaji mradi wa mawasiliano

Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile ameipongeza Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) kwa kusimamia kwa mafanikio utekelezaji wa miradi ya kimkakati inayoendelea kuboresha sekta ya usafiri wa anga nchini.



Ameyasema hayo leo wakati akikagua Mradi wa Mawasiliano ya Sauti baina ya Rubani na Muongozaji Ndege (VHF), ulioko wilayani Munduli, mkoani Arusha, ambako amesema TCAA imeonesha dhamira ya kweli katika kuboresha huduma za anga, jambo linaloongeza usalama na ufanisi katika usafirishaji  

Imeelezwa kuwa mradi huo wa VHF umegharimu Sh. Bilioni 31.6 na unatekelezwa katika vituo vikubwa 18 na vituo visaidizi 12 kote nchini. Huku Meneja wa Mradi, Mhandisi Francis Chale, akisema utekelezaji umefikia asilimia 90 na tayari baadhi ya vifaa vimeanza kufanya kazi katika kipindi cha majaribio.

“Mradi huu ni miongoni mwa hatua muhimu zinazolenga kuimarisha miundombinu ya usafiri wa anga kwa kutumia teknolojia ya kisasa. Tunaamini utasaidia kuongeza ufanisi na kupunguza changamoto zilizokuwa zikijitokeza awali,” amesema Mhandisi Chale.

Katika ziara hiyo, Kihenzile pia ametembelea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), ambako ameshuhudia mazingira ya kazi ya waongozaji ndege na namna miundombinu mipya inavyorahisisha kazi zao.

“Hatua hizi ni sehemu ya maono ya serikali katika kuhakikisha Tanzania inakuwa kitovu cha usafiri wa anga katika ukanda huu wa Afrika. Kufuatia ufungaji wa rada nne za kisasa za kuangazia anga, sasa tunaongeza uwezo wa mawasiliano ya moja kwa moja na rubani, hatua inayoinua kiwango cha usalama na udhibiti wa anga letu,” amesema Kihenzile.