Madiwani Shydc wapitisha rasimu ya sheria ndogo mpya

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 10:42 AM Jun 19 2025
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Ngassa Mboje akizungumza kwenye kikao cha Madiwani.
Picha: Marco Maduhu
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Ngassa Mboje akizungumza kwenye kikao cha Madiwani.

Rasimu hiyo imepitishwa jana Juni 18, 2025, katika kikao maalumu cha Baraza la Madiwani kilichoitishwa kwa ajili ya kujadili ajenda moja ya kupitisha mabadiliko hayo.

Awali, Wakili wa Serikali wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Salehe Hassan, akiwasilisha rasimu hiyo, amesema sheria ndogo wanazozirekebisha ni za mwaka 2018 ambazo zimeshapitwa na wakati, huku akieleza kuwa kuna vyanzo vipya vya mapato 19 ambavyo havikuwapo kwenye sheria hizo.

"Rasimu iliyopitishwa ni ya mwaka 2025, lakini sheria tunazozirekebisha ni za mwaka 2018. Baada ya hatua hii, rasimu itapelekwa kwa Mkuu wa Mkoa, kisha kwa Waziri mwenye dhamana, ndipo sheria hizo zitaanza kutumika rasmi," alisema Hassan.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Ngassa Mboje, baada ya kuwasilishwa kwa rasimu hiyo na kujadiliwa na madiwani, aliwauliza kama wameridhia ambapo kwa kauli moja walitamka kuwa wameipitisha.

“Sheria hizi ndogo ni uhai wa halmashauri,” alisema Mboje.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Dk. Kalekwa Kasanga, alisema sheria hizo zitaboresha uendeshaji wa shughuli za halmashauri na kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani.

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro, alisema madiwani hao wamefanya jambo la maana sana kwa kupitisha rasimu hiyo na kuiacha halmashauri ikiwa katika hali nzuri.

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga Vijijini, Edward Ngelela, aliwasisitiza watendaji kwamba sheria hizo zitakapoanza kutumika wazisimamie pamoja na kuhakikisha ukusanyaji wa mapato unafanyika kwa uaminifu.