Mahakama Kuu kusikiliza maombi ya rufaa dhidi ya mfanyakazi wa benki

By Grace Gurisha , Nipashe
Published at 05:55 PM May 07 2025
 Mahakama Kuu kusikiliza maombi ya rufaa dhidi ya mfanyakazi wa benki
Picha: Mtandao
Mahakama Kuu kusikiliza maombi ya rufaa dhidi ya mfanyakazi wa benki

Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, inatarajiwa kusikiliza maombi ya kuongeza muda wa kukata rufaa dhidi ya mfanyakazi wa benki, Ibrahim Masahi, anayetuhumiwa kumjeruhi jirani yake kwa nyundo. Tukio hilo linadaiwa kutokea baada ya mzozo uliotokana na malalamiko ya kumwagia maji machafu. Kesi hiyo itasikilizwa Juni 17, 2025, saa nne asubuhi, mbele ya Jaji Mfawidhi Salma Maghimbi.

Masahi anatuhumiwa kuwa Januari 11, 2023, katika eneo la Mbezi Msakuzi, Wilaya ya Ubungo, jijini Dar es Salaam, alimpiga jirani yake, Deogratus Minja, kwa nyundo na kumsababishia majeraha makubwa.

Hata hivyo, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni ilimuachia huru Masahi baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha shtaka hilo pasipo shaka. Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu Mkazi Amos Rweikiza, ambaye alieleza kuwa ushahidi haukuonyesha wazi jinsi mshtakiwa alivyotambuliwa usiku wa tukio.

Upande wa mashtaka uliwasilisha kusudio la kukata rufaa kupinga hukumu hiyo, ukidai kuwa shahidi wao alieleza kutambua mshtakiwa kutokana na mwanga wa kutosha wa taa za nje.

Kwa sasa, Jamhuri imewasilisha maombi ya kuongezewa muda wa kukata rufaa, ambapo Masahi kupitia wakili wake amejibu kwa kiapo kinzani.

Katika kesi ya msingi, Daktari Bingwa wa Mifupa kutoka MOI, Joel Mwinza (44), alieleza kuwa alipokea Minja akiwa na majeraha mbalimbali kichwani, mgongoni, mkononi na kisogoni, na alilazimika kumfanyia uchunguzi kwa kutumia X-ray na CT Scan.

Minja, katika ushahidi wake, alidai kuwa saa 2:30 usiku wa tukio, alipokuwa akipita nje ya geti la jirani yake Masahi, alikutana na kijana wa jirani huyo aliyemzuia kupita. Baada ya mazungumzo mafupi, Masahi alitoka nje na kumhoji Minja kuhusu kumshitaki kwa Serikali ya Mtaa, na baadaye kumshambulia kwa nyundo kichwani, hali iliyomlazimu Minja kukimbia akiomba msaada.