Mahakama yabariki Mchechu kulipwa bil 2.5/-

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 02:21 PM Jun 05 2025
Mahakama
PICHA: MTANDAO
Mahakama

Mahakama ya Rufani ya Tanzania jana imetoa uamuzi wake katika Rufaa Namba 658 ya mwaka 2023, iliyowasilishwa na Mwananchi Communications Ltd pamoja na Mhariri wa The Citizen Newspaper dhidi ya Nehemia Kyando Mchechu, na kutupilia mbali maombi hayo kwa kukubaliana na maamuzi ya Mahakama Kuu yaliyotolewa Machi 3, 2023.

Katika uamuzi huo uliotolewa mbele ya jopo la Majaji watatu - Jaji Rehema Kerefu, Jaji Omar Othman Makungu na Jaji Dk. Benhajj Masoud - Mahakama ya Rufani ilipitia hoja mbalimbali ikiwemo:Iwapo Mahakama Kuu ilikuwa na mamlaka ya kusikiliza shauri hilo, Iwapo mdai (Mchechu) aliweza kuthibitisha madai yake ya kudhalilishwa, Iwapo Mahakama Kuu ilitumia utaratibu sahihi kutoa nafuu na fidia.

Nehemia Mchechu


Majaji walikubaliana na hoja za wakili wa upande wa Nehemia Mchechu, Wakili Aliko Harry Mwamanenge, na kueleza kwamba Mahakama Kuu ilikuwa na uwezo wa kusikiliza shauri hilo, na kwamba mdai aliwasilisha ushahidi thabiti kuthibitisha kuwa alidhalilishwa. Pia, Mahakama Kuu ilifuata misingi sahihi ya kisheria katika kutoa nafuu na fidia.

Kwa msingi huo, Mahakama ya Rufani imethibitisha maamuzi ya Mahakama Kuu na kuitaka Mwananchi Communications Ltd kumlipa Bw. Nehemia Kyando Mchechu kiasi cha shilingi bilioni 2.5 kama fidia kwa kumdhalilisha pamoja na gharama nyingine kama ilivyoamuliwa awali.