Katibu wa NEC,Itikadi, Uenezi na Mafunzo CCM Taifa, Amos Makalla, amesema nchi za Tanzania na Kenya zinategemeana kutokana na kuchagizwa na amani na utulivu, akiwataka wananchi walioko mipakani kutumia fursa hiyo kuongeza biashara kujiimarisha kiuchumi.
Akihutubia leo Juni 9, 2025, katika mkutano wa hadhara uliofanyika Tarakea, wilayani Rombo, mkoani Kilimanjaro, akiendelea na ziara yake mikoa ya Kaskazini, Makalla amesema:
“Watu wetu wanafanya biashara kati ya Tanzania na Kenya tuwapongeze Rais wetu Samia Suluhu Hassan Rais wa Kenya, William Ruto, kuendeleza huu uhusiano mzuri. “Leo Tarakea imeendelea kukua inachagizwa na mwingiliano wa biashara kati ya Kenya na Tanzania, viongozi wetu hawa wanaendelea kuimarisha uhusiano wetu ambao ulijengwa na waasisi wa mataifa haya,” ameema.
Makalla amesema Wakenya wanakwenda Tanzania kulima vivyo hivyo kwa Watanzania, akisisitiza nchi hizo zinategemeana kutokana na kuchagizwa na amani na utulivu.
Hivyo, amewaeleza wananchi wa Tarakea kuwa wao ni mabalozi kati ya mpaka wa Tanzania na Kenya, hivyo waendelee kutumia fursa zipatikanazo katika mpaka, kuimarisha na kuongeza biashara kujiimarisha kiuchumi wa mtu mmoja mmoja, kikundi na taifa kwa ujumla.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED