Makalla amtaka Ulega kula sahani moja na wazembe

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 09:36 AM Apr 11 2025
KATIBU  wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa, CPA Amos Makalla akiwa Lindi.
PICHA: ROMANA MALLYA
KATIBU wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa, CPA Amos Makalla akiwa Lindi.

KATIBU wa NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa, CPA Amos Makalla, ameridhishwa na ujenzi wa daraja Somanga-Mtama,Wilaya ya Kilwa, mkoani Lindi, na kumtaka Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, kula sahani moja na wazembe.

Amemtaka pia, kuhakikisha madaraja yanayojengwa yawe katika kiwango cha ubora unaoendana na thamani ya fedha zilizotengwa na serikali kwa ajili hiyo.

Akizungumza jana Aprili 10, 2025 mara baada ya kukagua ujenzi wake unaoendelea, Makalla ambaye ameanza ziara ya siku 10 mikoa ya Lindi na Mtwara,  anasema baada ya changamoto hiyo kutokea, alisikia namna Waziri Ulega akifoka katika eneo hilo la tukio.

Kutokana na kadhia hiyo, Makalla ametoa pole kwa watumiaji wote wa barabara hiyo ya Kusini ambayo hutumiwa kusafirisha bidhaa mbalimbali.

“Haya yanayojitokeza si mambo ya kutengenezwa na binadamu, yanaweza kutokea mahali popote. Hata Marekani tunasikia madaraja, Ulaya tunasikia barafu au kimbunga,  ni mambo ambayo yako nje ya uwezo wa binadamu.

“Nilisikia Waziri akifoka hapa, na mimi nilielewa kwamba kwa nini anafoka. CCM ndicho chama chenye mkataba na wananchi na Rais Samia Suluhu Hassan ni Rais na Mwenyekiti wa CCM.

“ Kwa hiyo niliona hisia zake kwa watendaji wa wizara, niliona namna ambavyo aliamua kwamba ‘mimi ninapiga kambi hapa kuhakikisha tunarejesha mawasiliano’ ninakupongeza sana, ndivyo viongozi wanavyotakiwa kuwa, “anasema.

Makalla alimweleza Waziri huyo kwa kuwa anapigania maslahi ya wananchi aendelee, kwa sababu wao hawapiganii maslahi ya wazembe, na kumtaka aliowakemea ale nao sahani moja.

“Sisi tuko na wananchi, tuna dhamana na wananchi ndio maana kabla sijaongea na wananchi nimekuja kuona madhila haya kujiridhisha. 

“Nimeridhishwa na namna hatua mlizochukua Wizara ya Ujenzi na serikali Mkoa wa Lindi mmepiga kambi mpaka sasa tunapita,” anasema.

Naye, Waziri Ulega anasema serikali imetoa zaidi ya Sh. bilioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa madaraja 13.

Amekishukuru CCM kwa kutembelea maeneo yaliyopata tatizo hilo, akieleza Watanzania walilala hapo kwa muda wa siku mbili na ndipo magari yakaruhusiwa baada ya ukarabati wa dharura kufanyika.

Kadhalika, amesema Rais Samia amewapa maelekezo ya kufanya marekebisho ya barabara hiyo, hivyo katika bajeti ya 2025/26 wataikata kwa sehemu zilizoharibika na kujenga upya ili ikae sawa.