Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Khamis Khamis, ametoa wito kwa Watanzania kuendelea kutunza mazingira ili kukabiliana na changamoto ya kuenea kwa hali ya jangwa na ukame nchini.
Ametoa wito huo Juni 17, 2025, wakati akitoa hotuba kwenye kilele cha maadhimisho ya Siku ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Jangwa na Ukame Duniani, maadhimisho ambayo kitaifa yamefanyika mkoani Shinyanga.
Alisema ni jukumu la kila Mtanzania kuyatunza mazingira ili kukabiliana na hali ya jangwa na ukame katika kulinda mazingira kwa mustakabali wa taifa.
“Wananchi waongeze jitihada za kupanda miti hasa ile inayostahimili ukame, waache kukata miti hovyo na kuchoma mkaa kwa ajili ya kupikia. Tunawasihi watumie nishati safi ili kuokoa mazingira yetu,” alisema Khamis.
Aidha, amewataka wakulima, wafugaji na wachimbaji wa madini kuhakikisha kuwa shughuli zao haziwi chanzo cha uharibifu wa mazingira, ikiwemo ukataji miti usiozingatia sheria na taratibu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Julius Mtatiro, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, aliwaonya wananchi wa mkoa huo dhidi ya ukataji miti ovyo, akisisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa kwa watakaobainika kuharibu mazingira.
“Bado kuna wananchi wanaendelea kukata miti, hivyo sheria zipo wazi. Hatutasita kumchukulia hatua yeyote atakayebainika kuharibu mazingira,” alisema Mtatiro.
Aidha, alisema katika mkoa huo kuna kampeni ambazo zinaendelea za utunzaji wa mazingira pamoja na kupanda miti, na kwamba Shinyanga ya sasa siyo ile ya zamani ambayo ilikuwa haina miti kabisa, lakini sasa hivi kuna uhafadhari ambapo miti mingi imepandwa.
Kauli mbiu ya Siku ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Kuenea kwa Hali ya Ukame Duniani mwaka huu 2025 inasema: “Ongoa Ardhi, Kufungua Fursa.”
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED