Tanzania iko mbioni kuwa kitovu cha usambazaji wa nishati safi katika eneo la Afrika Mashariki, kufuatia uzinduzi wa mradi wa Kituo cha gesi ya kupikia majumbani (LPG) cha Tanga, kilichoanzishwa na kiongozi wa kimataifa wa gesi ya LPG, Petredec, kwa ushirikiano na Kampuni ya ASAS Group ya Tanzania.
Mradi huo umezinduliwa leo unatarajiwa kuwa kituo kikubwa zaidi cha LPG kinachopatikana kwa uhuru nchini, jambo ambalo ni hatua muhimu inayochangia usalama wa nishati na ajenda ya kupunguza matumizi ya kuni na kuchochea matumizi ya nishati safi chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Kituo hicho kipo katika eneo la hekta 26 Chongoleani, Ghuba ya Tanga, na kitakuwa mlango wa muhimu kwa ajili ya kuingiza gesi ya LPG Tanzania na nchi za jirani za Afrika Mashariki.
Baada ya kukamilika, kituo hicho kitakuwa na mabomba sita makubwa ya kuhifadhia LPG yenye uwezo wa jumla wa kuchukua mita za ujazo 40,000 katika awamu ya kwanza, pamoja na maeneo manane ya kupakia lori na bomba la chini ya bahari lenye urefu wa kilomita 2.8.
Kituo hiki pia kitaweza kushughulikia meli kubwa za gesi aina ya Very Large Gas Carriers (VLGCs), jambo ambalo Bandari za Tanzania kwa sasa haziwezi kufanya, hivyo kupunguza utegemezi wa Bandari ya Dar es Salaam iliyojaa mizigo.
Akizungumza huo, Jonathan Fancher, Mkurugenzi Mtendaji wa Petredec Global, alifafanua kuwa kituo hiki kitabadilisha usambazaji wa nishati katika ukanda huu.
“Historia imeonyesha kuwa miundombinu mikubwa ni msingi wa usambazaji wa LPG unaotegemewa na unaoshindana kwa bei,” alisema.
Aliongeza kuwa “Tunajivunia tena kuchangia maendeleo ya ukanda huu na tuna imani kuwa Kituo cha LPG cha Tanga kitasaidia kuifanya Tanzania kuwa kitovu kikuu cha nishati safi katika eneo la Afrika Mashariki.”
Mradi huu unaendana na malengo ya serikali ya kuongeza upatikanaji wa suluhisho la nishati safi ya kupikia hasa maeneo ya vijijii ambayo bado yanategemea mkukata miti kwa ajili ya kuni na mkaa, hali inayochangia uharibifu wa mazingira.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko ambaye alimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan aliipongeza Petredec na ASAS kwa uwekezaji mkubwa na muhimu kwa nchi wenye mchango mkubwa kwa maendeleo ya mtu mmoja na taifa kwa ujumla.
“Kutokana na malengo yetu ya kuongeza upatikanaji wa kupikia kwa njia safi kwa Watanzania wote, tunafurahia kumkaribisha Petredec na ASAS kama mwekezaji katika sekta ya LPG,” alisema Dk. Biteko.
Alisema uzinduzi huo ni uthibitisho ulio wazi kuwa serikali inatoa ujasiri kwa wafanyabiashara na uhakika kuwa baada ya uwekezaji wao, watapata faida na kuchangia kipato cha taifa.
Alisema uwekezaji kwenye sekta ya nishati, kwa miaka yote haujazidi dola 500 za Kimarekani , jambo ambalo uwekezaji huo mpya umebadilisha historia hiyo na kufanya uwekezaji wa dola milioni 100 za Kimarekani.
“Katika bilioni 4 dola za Kimarekani, tulizozitenga kwa ajili ya sekta binafsi, tayari tumeshapata milioni 100 maana yake tunatafuta bilioni 3.9 kutoka kwa wawekezaji wengine,” aliongeza Dk.Biteko.
Dk Biteko alisisitiza: “Pamoja na ajira 320,000 zitakazotengenezwa, na mpango wa kuongeza ajira 2000 kwa Watanzania wote, nataka niwaombe sana wawekezaji kuangalia utaratibu wa kutotafuta wafanyakazi kutoka nje wakati wapo wapo Watanzania wenye uwezo wa kuzifanya.”
Alisema kuongeza kasi ya awamu inayofuata ni muhimu ili LPG ifikie sehemu zote za nchi yetu na hata zaidi. Kuongeza uwezo wa kuingiza bidhaa ni hatua muhimu kuelekea kufanikisha mipango yetu ya kupanua suluhisho hili la nishati, aliongeza.
Kutokana na ongezeko kubwa la mahitaji ya LPG katika maeneo ya mijini na pembezoni mwa miji Afrika Mashariki, Kituo cha LPG cha Tanga kinatarajiwa kusaidia kusawazisha usambazaji na pia kuboresha bei na uhakika wa upatikanaji mambo muhimu yanayochochea matumizi ya nishati safi nyumbani.
Uwezo wa kituo hiki wa kufunguliwa kwa watumiaji wengi utawezesha mashirika mbalimbali kunufaika, kuanzisha soko lenye ushindani, kuhamasisha ubunifu na kupunguza bei kwa watumiaji.
Mkurugenzi Mtendaji wa ASAS Group of Companies, Naif Jaffer Abri, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Kampuni yake na Petredec katika kutoa suluhisho hili la nishati lenye mabadiliko makubwa.
“Kituo cha LPG cha Tanga ni mfano wenye nguvu wa jinsi makampuni makubwa mawili yanavyoweza kuunganisha nguvu zao za ndani na za kimataifa kuleta mradi wenye maana na wenye kuhamasisha,” alisema.
“Kitabakia kuwa kumbukumbu kubwa katika historia ya Taifa letu na kinatoa ahadi ya upatikanaji wa kupikia kwa njia safi kwa kaya kote nchini.”
LPG inatambuliwa kuwa suluhisho la haraka na bora zaidi la kupikia kwa jamii zisizo na umeme, ambazo ni nyingi katika nchi za Afrika Mashariki. Kama gesi yenye moshi mdogo na yenye ufanisi, LPG pia hutoa njia ya kupunguza uchafuzi wa hewa ndani ya nyumba na kuboresha afya hasa kwa wanawake na watoto.
Baada ya kumaliza ujenzi wa barabara za kufikia eneo la kituo na kuidhinisha mkataba wa Uhandisi, Ugavi na Ujenzi (EPC), Petredec na ASAS wako tayari kuanza ujenzi wa awamu kubwa wiki chache zijazo.
Kituo hicho kinatarajiwa kukamilika kufikia mwishoni mwa mwaka 2027, na baada ya hapo kitakuwa mchezaji mkuu katika usambazaji wa LPG Tanzania na ukanda mzima wa Afrika Mashariki.
Alisema kituo cha LPG cha Tanga siyo tu mradi mkubwa wa miundombinu ni hatua muhimu katika kufanikisha mabadiliko ya nishati Tanzania, likitoa msingi wa ukuaji wa uchumi, maendeleo ya viwanda, na kuboresha maisha ya mamilioni ya wananchi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED