Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amesikia kilio cha wasafirishaji wanaotumia pikipiki na bajaji za miguu mitatu zinazotumia nishati ya umeme kwa kupunguza gharama za leseni kutoka Shilingi 80,000 hadi Shilingi 30,000.
Hayo yamesemwa jijini Dar es Salaam na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, wakati wa ufungaji wa mafunzo kwa madereva hao wa maguta yaliyofanyika katika Chuo cha Polisi.
DC Mpogolo amesema usikivu wa Rais Samia Suluhu Hassan umeendelea kuhakikisha vilio vya madereva wa vyombo vya moto vinasikilizwa na kupatiwa ufumbuzi ili waweze kufanya shughuli zao kwa amani.
Ameeleza kuwa kutolewa kwa mafunzo hayo na Jeshi la Polisi kutasaidia kuongeza uelewa na usalama, pamoja na kutambulika rasmi kama familia kwa kusajiliwa, tofauti na awali ambapo hawakuwa na leseni na hawakujulikana kwa urahisi.
Amesema punguzo hilo limekuja ikiwa ni mwezi mmoja toka atangaze kuwa madereva hao kutoka maeneo mbalimbali wanasajiliwa ili kuwawezesha kufanya shughuli zao vizuri katikati ya jiji kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu watakazowekewa ili kupunguza msongamano katika masoko.
Wakati huohuo, DC Mpogolo amewakumbusha vijana kutumia muda wao vizuri kwa kufanya kazi kwa weledi ili waweze kusaidia familia zao na kutoa mchango wa maendeleo kwa Serikali, kwa kuwa kazi ni msingi wa utu.
Madereva hao wamepata mafunzo kutoka Jeshi la Polisi kwa kufundishwa misingi ya kazi, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuwasajili na kuwatambua rasmi katika sekta ya usafirishaji, na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) kuwapa leseni ili wafanye kazi kwa amani wakiwa barabarani.
"Nawaasa tumieni vizuri fursa hii kuboresha kazi zenu mnazofanya kutumia nishati safi, kufanya kazi kwa uaminifu, usalama wa dereva na chombo chake, na kuwa na mahusiano mema kwani dunia ya sasa inafanya kazi kwa mtandao na wateja wanataka mizigo ifike haraka kwa kutumia usafiri wa uhakika na salama," amesisitiza Mpogolo.
Aidha, Mpogolo ametoa shukrani kwa Jeshi la Polisi linaloongozwa na IGP Camillus Wambura kwa kukubali ombi la kufanyika kwa mafunzo kwa madereva hao wa maguta ya umeme kwa kupunguza gharama za masomo kutoka Shilingi 100,000 hadi Shilingi 40,000.
Kwa upande wao, madereva hao wameiomba Serikali iwasaidie kuangalia na kupunguza bei ya betri za maguta na kutafutiwa maeneo ya maegesho mjini. Pia wameomba kushughulikiwa kwa suala la vipuri kwa kuhakikisha wawekezaji wanawekeza nchini ili kuondoa madalali wanaoongeza bei za vifaa na kudhibiti upandishwaji wa bei.
Mafunzo hayo yamefanyika ikiwa ni mwezi mmoja tangu Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, na Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Elihuruma Mabelya, walipokutana na madereva hao katika viwanja vya Mnazi Mmoja na kuwataka kusajiliwa ili watambulike rasmi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED