Mbunge wa Viti Maalum, Dk. Thea Ntara (CCM), anayewakilisha Taasisi za Elimu ya Juu na Vyuo Vikuu Nchini, ameitaka serikali kutazama kwa jicho la tatu, stahiki za mafao ya Wahadhiri wa Vyuo Vikuu, ambao ni maprofesa wasimamizi wa vyuo.
Akichangia jana Bungeni Jijini Dodoma, mjadala unaoendelea wa Hotuba ya Bajeti ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu, kwa Mwaka wa Fedha 2025/2026, Dk. Thea amesema:
“Lakini pamoja na hayo, nisisahau hili jambo. Kuna jambo lile nimelizungumza leo (Aprili 14, 2025) ni mara ya tatu, kuhusu mafao ya wakuu wa vyuo vikuu.
“Mheshimiwa Lukuvi (William) unanisikia hapa, hili jambo tumeliongea, hao wakuu wa vyuo wamekaa wanasubiri, wanasema wanaambiwa liko kwenye meza liko kwenye meza.
Niwaombe mkalichukue hapo kwenye meza mlishike mkononi, mlimalizie hilo suala la mafao ya vyuo vikuu.
Zaidi ameeleza Dk. Thea, “Juzi, juzi kuna mafao yale ya watu wa vyeti feki, mlilifanyia kazi haraka sana, lakini hawa Wahadhiri wa Vyuo Vikuu, ambao ni maprofesa wasimamizi wa vyuo, bado mpaka leo hii, hivi ninavyoongea haijulikani nini kinaendelea.”
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED