SERIKALI na Sekta binafsi zimeombwa kutenga vyumba maalum kwa ajili ya watu wanaokabiliwa na changamoto ya akili, ili waweze kujieleza na kupata msaada unaohitajika.
Ombi hilo limekuja kutokana na ongezeko wa watu wengi hususani wanawake kupata tatizo hilo, wamesema ni muhimu kuwa na maeneo maalum kwa ajili ya watu kujadili na kushughulikia.
Vilevile viongozi wameombwa kuwaruhusu kubaki au kwenda nyumbani watu wenye changamoto hiyo ili kupata nafasi ya kushughulikia jambo linawalowasibu na Serikali imeshauriwa kuunda sera itakayoweka kipaumbele katika kushughulikia masuala ya afya ya akili, ili kusaidia watu wengi kupata suluhu ya changamoto zinazowakabili.
Ombi hilo lilitolewa jana na Mchechemuzi wa masuala ya Afya ya Akili nchini, Mariam Surve, wakati akiwasilisha mada kuhusu jinsi wanawake wanavyoweza kukabiliana na matatizo ya afya ya akili.
Mada hiyo iliwasilishwa katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake yaliyoandaliwa na Shirika la Plan International nchini.
Mariam Surve Ames idiot a kwamba wanawake wanaposherehekea mafanikio yao, wanapaswa pia kutambua na kushughulikia matatizo ya akili ambayo yanaathiri kundi hilo.
"Ni muhimu kwa wanawake kuweka kipaumbele afya zao ili kuwa bora kazini na nyumbani, jamii inapaswa kuwaunga mkono wanawake hawa kwa kuwajali na kuwahimiza kuzungumza kuhusu changamoto zao, kwani ni njia mojawapo ya kupata msaada,” amesema Mariam.
Ameongeza kuwa wanawake wanapokutana na changamoto za akili, ni muhimu kuwaona wataalamu wa saikolojia kwa ushauri na nasaha, kwani afya ya akili ni kipaumbele kwa kila mtu.
Katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Programu wa Shirika la Plan International, Peter Mwakabwale,ameeleza kuwa bado kuna umuhimu wa juhudi za ziada katika kupambana na ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake.
Amesema ingawa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) yanataka kufikia usawa wa kijinsia ifikapo mwaka 2030, Plan International imejipanga kuwafikia wanawake milioni 200 ifikapo mwaka 2027 kwa kuwajengea uwezo katika eneo la kuongoza, kujifunza, kuamua na kustawi ili kupambana na ukatili wa kijinsia.
Mwakabwale ameongeza kuwa shirika hilo linatekeleza miradi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kila mtoto wa kike anamaliza shule, ujenzi wa vyoo na vyumba maalum vya hedhi, pamoja na vifaa muhimu kama sketi kwa ajili ya kusaidia Watoto hao.
Sofia Mbeyela, amezungumzia ushiriki wa wanawake wenye ulemavu katika jamii, alisema ni muhimu jamii iamini uwezo wa wanawake wenye ulemavu bila kujali hali zao, kwani hii itasaidia kuondoa mtazamo hasi wa kuwaona hawawezi kushiriki kwenye shughuli za kijamii.
Amehimiza hatua za kuchukua ili wanawake wenye ulemavu waweze kupata fursa sawa na wanawake wengine ni kuunda sauti ya pamoja ambayo itasaidia kundi hilo kujitokeza na kuonyesha uwezo wao.
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Plan International Tanzania, Jane Sembuche amewahamasisha wanawake kufanya kazi kwa bidii na wasite tamaa katika kupambana kufikia ndoto zao.
Vilevile amewataka kujitahidi katika nafasi waliaminiwa kuongoza au kufanya kazi kuongeza thamani ya vitu wanavyofanya ili watu watambue umuhimu wao.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED