Maandalizi ya kuwasha Mwenge wa Uhuru Pwani yafikia hatua nzuri

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 06:30 PM Mar 12 2025
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete.
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete, amekagua maandalizi ya uwanja wa Shirika la Elimu Kibaha, mkoani Pwani, utakaotumika kuwasha Mwenge wa Uhuru Aprili 2, 2025.

Baada ya ukaguzi huo, Waziri Kikwete amesema ameridhishwa na maendeleo ya maandalizi, huku akihimiza kasi iongezwe ili kukamilisha kazi kabla ya muda uliopangwa. Aidha, amepongeza maandalizi ya vijana wa halaiki wanaoendelea na mazoezi kwa ajili ya tukio hilo kubwa la kitaifa.

Akizungumzia ujumbe wa Mwenge wa Uhuru 2025, amesema unalenga kuhamasisha wananchi kutumia haki yao ya msingi ya kupiga kura Oktoba 2025, kupinga rushwa, kutunza afya, na kuzingatia kilimo chenye tija huku wakidumisha umoja wa kitaifa.

Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, amesema maandalizi ya uwanja huo yamefikia asilimia 70 na wanatarajia kukamilisha kazi hiyo ifikapo Machi 20, ikiwemo kuunganisha miundombinu ya umeme.

"Tumejipanga kikamilifu kwa ulinzi na maandalizi yote muhimu. Mwenge wa Uhuru utaanzia hapa Pwani, hivyo nawasihi wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki tukio hili muhimu," amesema Kunenge.