Watanzania 36 wahukumiwa kwa kuondoka nchini kinyume cha sheria

By Imani Nathaniel , Nipashe
Published at 08:51 PM Mar 12 2025
Watanzania 36 wahukumiwa kwa kuondoka nchini kinyume cha sheria
Picha: Imani Nathaniel
Watanzania 36 wahukumiwa kwa kuondoka nchini kinyume cha sheria

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imewahukumu Watanzania 36 kulipa faini ya shilingi 30,000 kila mmoja au kutumikia kifungo cha miezi mitatu jela kwa kosa la kuondoka nchini Tanzania kinyume cha sheria na kuingia Afrika Kusini bila vibali halali.

Hukumu hiyo imetolewa Jumanne, Machi 11, 2025, na Hakimu Mkazi Mwandamizi Geoffrey Mhini, baada ya kuridhishwa na ushahidi uliowasilishwa mahakamani.

Katika kesi hiyo namba 72/2024, Wakili wa Serikali, Raphael Mpuya, akisoma shtaka mbele ya Hakimu Mhini, alieleza kuwa watuhumiwa 36, akiwemo Said Omary Buba (25) mkazi wa Kizuiani, Dar es Salaam, Allen Ernest William (21) mkazi wa Mwanza, Hamad Said Magimaba (25), na wenzao 33, walitumia usafiri wa barabara kupita katika mipaka isiyojulikana hadi Afrika Kusini.

Wakili Mpuya alieleza kuwa watuhumiwa hao waliingia Afrika Kusini bila kufuata taratibu rasmi za uhamiaji, bila hati za kusafiria (passport), na bila kupitia ukaguzi wa maofisa wa uhamiaji, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Baada ya kuingia nchini humo, watuhumiwa waliendelea kuishi Afrika Kusini hadi walipokamatwa katika misako na doria kwa nyakati tofauti na kushikiliwa kwenye magereza mbalimbali nchini humo. Machi 5, 2025, walirudishwa Tanzania kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), ambapo waliwekwa chini ya ulinzi wa maofisa wa uhamiaji kwa tuhuma za kuondoka nchini kinyume cha sheria.

Katika maelezo yao, watuhumiwa walikiri kuondoka Tanzania bila kufuata taratibu. Wakili wa utetezi, Godfrey Mpandikizi, aliiomba mahakama ipunguze adhabu kwa wateja wake, akieleza kuwa walilazimika kuondoka nchini kwa sababu ya ugumu wa maisha na ukosefu wa ajira.

Baada ya kusikiliza pande zote, Hakimu Mhini alitoa hukumu ya kulipa faini ya shilingi 30,000 kila mmoja au kutumikia kifungo cha miezi mitatu jela.

1