Wananchi wa Mtaa wa Tegeta "A" katika Manispaa ya Ubungo, jijini Dar es Salaam, wamejitokeza kwa wingi na kuelekea ofisi za Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa huo wakipaza sauti zao kupinga ongezeko la nauli kutoka shilingi 500 hadi 1,000 kwa wanaotumia usafiri wa Daladala na Bajaji za kuchangia.
Wakizungumza kwa hasira, wananchi hao wamesema kupanda kwa nauli kumewaathiri kwa kiasi kikubwa, hasa wafanyakazi wa kipato cha chini na wanafunzi wanaotegemea usafiri huo kila siku.
Akijibu malalamiko yao, Mwenyekiti wa Mtaa huo, Protus Ruwanda, amesema kupanda kwa nauli kumetokana na hali mbovu ya miundombinu, hususan barabara, hali inayoongeza gharama za uendeshaji kwa watoa huduma za usafiri.
"Tunaendelea kufanya mawasiliano na mamlaka husika ili kuona namna ya kuboresha barabara hii. Hata kama si kwa kuweka lami mara moja, basi angalau ikwanguliwe ili kupunguza athari kwa wananchi, hasa katika kipindi hiki cha mvua," amesema Ruwanda.
Kwa muda mrefu, wakazi wa Tegeta "A" wamekuwa wakichangia fedha zao kwa ajili ya matengenezo ya barabara, huku ahadi za Serikali za kuiwekea kiwango cha lami zikisubiriwa kwa muda mrefu bila utekelezaji. Wananchi sasa wanaitaka Serikali kuchukua hatua madhubuti ili kuondoa kero hii ya muda mrefu, wakisema kuwa kupanda kwa nauli ni mzigo mkubwa kwao katika hali ngumu ya kiuchumi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED