VIJANA wanne wakazi wa Dar es Salaam wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni, wakituhumiwa kuchepusha mizigo ya vifaa vya magari iliyokuwa ikielekea nchini Congo wao wakaipeleka eneo la Mikocheni.
Washtakiwa hao ni Athanas Msenye (45) Maria Said (37), Godfrey Chamali (31) na Polycap Haule (29), wanadaiwa kukwepa kodi na kuisababishia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hasara ya Sh 125.5, baada ya kuchepusha mizigo kinyume na sheria.
Mashtaka mengine ni kukwepa kodi kwa njia ya udanganyifu, kuchepusha mizigo kutoka kwenye njia iliyoidhinishwa, kutoa nyaraka ya uongo, kuondoa lakiri ya forodha, kuisababishia mamlaka hasara na kupatikana na mali au bidhaa ambazo hazijalipiwa ushuru wa forodha.
Akisoma hati ya mashtaka, Wakili wa Serikali John Mwakifuna akisaidiana na Wakili Auni Chilamula na Emmanuel mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Veneranda Kaseko wa Mahakama hiyo alidai kuwa washtakiwa wanatumiwa kwa mashtaka sita.
Ilidaiwa kuwa Februari 7, 2025 washtakiwa wakiwa eneo la Mikocheni ndani ya Wilaya ya Kinondoni walitoa nyaraka ya uongo kwamba mzigo unaohusu vifaa mbalimbali vya magari ilikuwa safarini kuelekea nchini Congo lakini wakaichepusha na kuilkezea eneo la Mikocheni Dar es Salaam hali ambayo ilisababisha ukwepa kodi wa zaidi ya Sh. 125,245,219.82
Katika shtaka la pili inadaiwa, siku na mahali hapo washtakiwa wote, walichepusha mzigo wa vifaa mbalimbali vya magari kutoka katika njia iliyokuwa imeidhinishwa kupita ya kutoka Dar es Salaam hadi Congo na wao wakaupeleka mzigo huo eneo la Mikocheni.
Washtakiwa Msenye na Amina pia wanadaiwa Februari 7, 2025 huko katika bandari ya Dar es Salaam walitoa tamko la uongo kuhusu maelezo ya mzigo wa vipuri vya gari na kushindwa kujimuisha taa na sola.
Inadaiwa kuwa Februari 7,2025 eneo la Tabata Mwananchi, washtakiwa waliondoa lakiri ya forodha kutoka kwenye kontena la gari.
Katika shtaka la tano inadaiwa washtakiwa wote kwa makusudi, walifanya kitendo cha kukwepa kodi na kuisababishia TRA hasara ya Sh. 125,245,219.81
Katika shtaka la sita inadaiwa kuwa Februari 7,2025 huko Mikocheni, washtakiwa Chamali na Haule walikutwa na vifaa mbali mbali vya gari huku wakijua kuwa vifaa hivyo havijalipiwa ushuru wa forodha na hivyo kukwepa kodi ya Sh. 125,245,219.82.
Hata hivyo washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi hadi itakapopewa kibali .
Kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi katika kesi hiyo bado haijakamilika na umedai kuwa dhamana ya washtakiwa iko wazi, wameiomba Mahakama kutoa dhamana kwa mujibu wa sheria na masharti mengine ambayo Mahakama itaona yanafaa.
Hata hivyo, Hakimu Kaseko amesema amezingatia washtakiwa wanatuhumiwa na kesi ya Uhujumu Uchumi na kwa kuwa Mahakama haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo hatatoa masharti ya dhamana hadi pale kibali cha kuisikiliza kitakapotolewa
Washtakiwa wamerudishwa mahabusu. Kesi hiyo itakuja kwa ajili ya kutajwa Machi 24, 2025.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED