WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema serikali inaendelea kusimamia utoaji wa huduma za maji safi na salama nchini ili kuhakikisha hali ya upatikanaji wa maji inawafikia wananchi kote nchini kwa asilimia 100.
Majaliwa amezingumza hayo leo wakati akiweka jiwe la msingi katika Mradi wa Upanuzi wa Mtandao wa Majisafi ya Ziwa Victoria kutoka Makomero hadi Mgongoro, uliopo kijiji cha Mwamayoka, Igunga mkoani Tabora ambao umegharimu Sh. milioni 840.8, ukitarajiwa kuwahudumia wananchi takribani 5,402.
“Mradi huu ni matokeo ya utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kuweni na uhakika kwamba Rais Samia Suluhu Hassan ni kiongozi anayewajali, anawapenda na anasikiliza changamoto zenu, endeleeni kutekeleza majukumu yenu ipasavyo kwasababu tunaye kiongozi madhubiti," amesema Majaliwa.
Ameongeza kwa kuiagiza Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kuongeza na kusogeza vituo vya kuchotea maji karibu na wananchi pamoja na hukakikisha miradi hiyo inatoa maji wakati wote.
Mradi huo ambao umefikia asilimia 80 ya ujenzi unahusisha ujenzi wa vituo sita vya kuchotea maji, ukarabati wa vituo sita vya kuchotea maji, ukarabati wa manywesheo mawili ya mifugo, kuchimba mitaro ya kulaza bomba na kufukia mitaro yenye mita 25,000.
Waziri Majaliwa yuko mkoani Tabora kwa ziara ya kikazi ya siku mbili.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED