SHAHIDI ASP Njama, amedai Fuso walilolikuta limepata ajali maeneo ya Chamakweza wilayani Chalinze, lilisheheni mikungu ya ndizi 80 na mifuko ya salfeti 83 yenye majani makavu yanayosadikiwa kuwa bangi chini ya ndizi.
ASP Njama amedai hayo Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi mbele ya Jaji Godfrey Isaya, wakati anatoa ushahidi wa upande wa mashtaka.
Mshtakiwa katika kesi hiyo, Raisan Mussa, anashtakiwa kwa kukutwa na viroba 83 vyenye majani yanayosadikiwa dawa za kulevya aina ya bangi.
Amedai walikuta Fuso lenye namba T223 ATC limepata ajali, maeneo ya Chamakweza Chalinze, wakatilia shaka kwa kuwa walikuwa na taarifa za siri kuhusu gari hilo.
Shahidi amedai walianza kupekua na baada ya dakika chache, Koplo George alisema juu kuna ndizi lakini chini kuna viroba vya mifuko ya salfeti akaamuru ndizi za juu zitolewe, zilishushwa zote, ilikuwa mikungu 80.
Anadai Koplo George alitoa majani kidogo kuangalia ikaonekana ni bangi aliamuru mifuko yote ya salfeti ishushwe chini na wakati vinashushwa vilikutwa viroba 83 vyenye majani makavu yadhaniwayo kuwa dawa za kulevya.
Mahakamani ilihamia nje, kwa ajili ya kutambua Fuso hilo na shahidi alilitambua.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED