Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Victoria Mwanziva, ameendelea na ziara yake ya kata kwa kata ndani ya wilaya hiyo, akifanya ukaguzi wa miradi ya maendeleo na kusikiliza changamoto za wananchi kwa lengo la kuzitatua.
Katika ziara hiyo, Mwanziva amekagua miradi ya afya, elimu na maji katika Kata ya Kitomanga, Manispaa ya Lindi, ikiwa ni pamoja na kufanya mkutano wa hadhara na wananchi wa eneo hilo.
Akiwa katika Kituo cha Afya Kitomanga, alikagua utoaji wa huduma katika wodi ya mama na mtoto na kutoa mahitaji muhimu kwa akina mama waliokuwa wamejifungua. Aidha, amefuatilia maendeleo ya ujenzi wa Shule ya Sekondari Kitomanga, ambayo imepokea zaidi ya shilingi milioni 515 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa, matundu ya vyoo na ukarabati wa mabweni. Amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha ubora wa mradi na matumizi sahihi ya fedha zilizotolewa.
Katika sekta ya maji, Mwanziva ameongoza ukaguzi wa mradi wa maji wa Nanjime katika Kijiji cha Mkwajuni, wenye thamani ya shilingi bilioni 1.052. Mkandarasi wa mradi huo alikuwepo na ameahidi kuendelea na utekelezaji kwa mujibu wa mkataba ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi na salama kwa wakati.
Ziara hiyo pia ilifika katika Shule ya Msingi Kingurungundwa, ambako alishiriki zoezi la upandaji wa miche 100 ya miti ya vivuli na matunda. Zoezi hilo ni sehemu ya kampeni ya utunzaji wa mazingira na lishe, kwa kuwa matunda hayo yatasaidia kuboresha lishe kwa wanafunzi.
Mwisho wa ziara hiyo, Mwanziva alifanya mkutano wa hadhara na wananchi wa Kitomanga, Kijiji cha Mkwajuni na Kitongoji cha Mjimwema, ambapo alisikiliza na kushughulikia changamoto zinazowakabili wananchi wa maeneo hayo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED