Majaliwa: Dhamira ya Rais Samia kila nyumba iwe na umeme

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 06:57 PM Mar 12 2025
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa.
Picha: Mpigapicha Wetu
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa.

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, amesema dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kila nyumba ya Mtanzania, iwe mijini au vijijini, inakuwa na umeme kwa gharama nafuu ili kuboresha maisha ya wananchi na kuchochea maendeleo.

Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Mwamayoka, Wilaya ya Igunga mkoani Tabora leo, ambako yuko katika ziara ya kikazi, Majaliwa amesema serikali imepunguza gharama za kuunganisha umeme hadi 27,000 ili kila Mtanzania aweze kumudu kuunganisha huduma hiyo muhimu.

"Rais Samia anataka kuona kila nyumba ya Mtanzania inawaka umeme. Amehakikisha gharama zinashuka hadi 27,000 ili kila mwananchi, hasa wa vijijini na vitongojini, aweze kumudu kuvuta umeme," amesema Majaliwa.

Ameeleza kuwa Mbunge wa Jimbo la Igunga, Nicholaus Ngassa, tayari amewasilisha orodha ya vijiji vyote vinavyohitaji umeme, na sasa vitongoji navyo vinaingizwa kwenye mpango huo ili kuhakikisha hakuna Mtanzania anayekosa huduma hiyo.

"Tunataka kuona kila nyumba inawaka umeme, bila kujali muundo wake iwe ni ya ghorofa, yenye bati au hata isiyokuwa na bati. Lengo ni kuhakikisha umeme unawafikia wote," amesema Majaliwa.

Majaliwa pia amewapongeza wataalamu wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kutafuta teknolojia rafiki kwa wananchi wa maeneo ya pembezoni.

Amesema kwa baadhi ya nyumba, ambazo hazihitaji kuunganishwa moja kwa moja na nyaya za umeme wa kawaida, kuna mfumo maalum utakaowawezesha kupata taa na huduma nyingine za msingi za umeme.

"Wataalamu wa TANESCO wameleta mfumo mzuri ambao unaruhusu baadhi ya nyumba kupata umeme bila hata kuunganishwa na waya moja kwa moja. Wanakuletea kifaa maalum ambacho kinawasha taa za nyumba nzima," amesema.