WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye mkesha mkubwa wa kuliombea Taifa, utakaofanyika Ijumaa hii, Machi 14, 2025, katika ukumbi wa Ubungo Plaza.
Lengo la mkesha huo ni kuliombea Taifa na Rais Samia Suluhu Hassan, katika kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2025 ili ufanyike kwa amani na utulivu.
Mkesha huo umeandaliwa na Kiongozi wa Kanisa la Heavenly Image Manifest (HIM) chini ya Nabii Edmund Mystic, katika ukumbi wa Ubungo Plaza, utakaonza saa 2:00 usiku na kuendelea.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 12, 2025 jijini Dar es Salaam, Nabii Edmund, amesema mkesha huo awali ulipangwa kufanyika Februari 28, mwaka huu na ukasogezwa mbele hadi Ijumaa hii.
Nabii Edmund amesema kwa Tanzania mwaka 2025 ni muhimu kwa Taifa kwasababu ya tukio kubwa la uchaguzi mkuu ambao utaamua hatma ya nchi kwenye utawala wa viongozi.
Amesema kanisa lina nafasi ya kulibeba Taifa kwa namna moja na nyingine kwa kufanya maombi hivyo yatahusisha pia kumwombea Rais Samia kwasababu yeye ni mtawala na amebeba hatima kubwa ya Watanzania.
"Habari ya kuombea Tanzania ni suala nyeti ambalo Mungu anaenda kuikumbuka nchi na kuirehemu, kama kuna makosa tumefanya alafu tukasimama kuomba rehema kwa Tanzania Mungu ana uwezo wa kufanya kitu, maombi ni kitendo cha unyenyekevu na tuna muhitaji Mungu aingilie kati katika haya,"amesema Nabii Edmund.
Amesema yanayoendelea nchini Congo si kwamba wananchi wake wanapenda, hivyo ni wajibu wa Watanzania na waombaji kuliweka Taifa mikononi mwa Mungu kwa maombi ili aghairi mabaya yote.
Edmund amesema kuwa waimbaji mbalimbali wa nyimbo za injili pamoja na watumishi wa Mungu kutoka makanisa mbalimbali nchini watakuwapo.
Amewataja baadhi ya waimbaji watakaoishiriki ni Upendo Nkone, Beatrice Mwaipaja, John Lisu, Kwaya ya Uinjilisti KKKT Kijitonyama na Kwaya ya Ufunuo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED