"Mtaa hautaki digrii, unataka ujuzi"- Faris Buruhan

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 09:26 PM Mar 12 2025
news
Picha: Mpigapicha Wetu
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Kagera, Faris Buruhan.

Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Mkoa wa Kagera, Faris Buruhan, amewataka vijana wanaopata mafunzo ya ufundi katika vyuo vya VETA kutumia vyema ujuzi wao, akisisitiza kuwa ajira mtaani zinategemea zaidi ujuzi na utendaji kazi badala ya vyeti vya elimu ya juu.

Faris ametoa kauli hiyo leo, Machi 12, 2025, alipokuwa akizungumza na wanafunzi wa Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Karagwe, ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku 16 mkoani humo.

Amesema elimu ya ufundi stadi ina nafasi kubwa katika maendeleo ya taifa, kwani kinachohitajika zaidi ni maarifa ya kiufundi na uwezo wa kubuni mambo yatakayowawezesha vijana kujiajiri au kuajiriwa kwenye sekta mbalimbali.

"Leo, mtaa hauhitaji digrii, PhD, wala vitabu vingi, bali unahitaji watu wa kuendesha mitambo viwandani. Mpango wa nchi ni kuwekeza kwenye viwanda, na wanaoendesha mitambo siyo wenye vyeti pekee, bali wale wenye maarifa na ujuzi wa ufundi," amesema Faris.

Aidha, amewahimiza vijana kusoma kwa bidii na kufanya kazi kwa weledi bila kujilinganisha na wengine kwa misingi ya kiwango cha elimu, akiwataka wajione mashujaa wa taifa kwa kuchangia maendeleo kupitia ujuzi wao wa kiufundi.

"Kwa sasa, elimu ya ufundi ndiyo kimbilio la vijana. Hakuna haja ya wale waliopo katika vyuo vya kati na ufundi stadi kujiona duni. Ni wakati wao kujivunia nafasi yao katika kulijenga taifa," ameongeza.