Lissu aeleza maumivu ya walioshindwa uchaguzi CHADEMA

By Enock Charles , Nipashe
Published at 04:22 PM Mar 12 2025
Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu akizungumza na waandishi wa habari wa Nipashe nyumbani kwake jijini Dar es Salaam.

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Tundu Lissu ameeleza kutambua maumivu ya walioshindwa uchaguzi ndani ya chama hicho na kutaja mikakati ya kutibu majeraha yaliyotokana na uchaguzi huo.

Akizungumza na waandishi wa Nipashe waliofika nyumbani kwake Jumapili iliyopita, Lissu alisema ameliachia Baraza la Wazee la Chama hicho (BAZECHA) kazi ya kuponya majeraha hayo ili kurejesha umoja ndani ya chama hicho.

“Tuna baraza la wazee ambao nimewapa jukumu la kusaidia kuponya majeraha, majeraha ya uchaguzi kama yalivyo majeraha mengine hayaponi siku moja” alisema Lissu.

“Kama hujawahi kushindwa uchaguzi huwezi kujua uchungu wa kushindwa uchaguzi” alisema.

 Lissu alikiri uchaguzi wa viongozi ndani ya chama hicho uliofanyika Januari 21 mwaka huu umeacha majeraha makubwa.

Mtaalam huyo wa sheria pia alikiri majeraha hayo yatachukua muda mrefu kupona kwa kuwa baadhi ya majeraha kwa namna yalivyo hayawezi kupona mara moja kwa haraka ingawa imani yake ni kuwa muda utayaponya.

"Uchaguzi wetu ulikuwa mkali sana. Nikikuuliza kama ulilala Januari 21 mwaka huu, utaniambia ulikesha kama nilivyokesha mimi. Taifa zima lilikesha kufuatilia uchaguzi wa CHADEMA. Sasa uchaguzi wa aina hiyo unakuwa na maumivu yake ukishindwa. Kwa hiyo kulikuwa na hiyo mikwaruzano, tumesema kwamba tuifanyie kazi na tunaifanyia kazi.