KAMISHNA Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Yussuf Mwenda, amesema waombaji 135,027 wamejitokeza kuomba nafasi za kazi 1,596 zilizotangazwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Amesema, wiki ijayo Mkurugenzi wa Utawala anatarajiwa kutoa utaratibu kuhusu ajira hizo.
Amesema hayo jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya miaka minne ya serikali ya awamu ya sita.
Kamishna Mkuu Mwenda, amesema kumekuwa na mwitikio mkubwa wa Watanzania kwenda kufanya kazi TRA na kuwahakikishia kuwa kila mtu ambaye ana sifa atapata fursa ya ajira ndani ya TRA.
“Wiki ijayo Mkurugenzi wa Utawala atatoa utaratibu, niwahakikishie Watanzania tunataka ‘best brain’ zije ndani ya TRA, ili kuongeza zaidi weledi, tutaweka mazingira ya haki na usawa,” amesema.
Hata hivyo, amesema Mamlaka hiyo imefanya jitihada kubwa kuhakikisha inatekeleza maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kurahisisha upatikanaji wa huduma bora kwa wateja kwa kusogeza huduma za kikodi karibu na wananchi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED